Auba airudisha Arsenal Europa league

Muktasari:

Kwa kubeba ubingwa huo Arsenal watacheza Europa msimu ujao nafasi ambayo hawakuwa nayo baada ya kumaliza nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi kuu England

London, England. Mabao mawili aliyofunga mshambuliaji, Pierre-Emerick Aubameyang kwenye mchezo wa Fainali ya Kombe la FA dhidi ya Chelsea kwenye Uwanja wa Wembley  yameifanya Arsenal kutwaa ubingwa wa Kombe la FA kwa mara ya 14.

Chelsea ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza dakika ya tano kupitia kwa Christian Pulisic ambaye alishindwa kumaliza dakika 90 za mchezo huo kutokana na kupata majeraha.

Bao hilo lilidumu kwa dakika 23, Arsenal wakasawazisha kupitia kwa Aubameyang ambaye alimfunga kipa wa Chelsea Willy Caballero kwa mkwaju wa penalty baada ya César Azpilicueta kumchezea rafu mshambuliaji huyo raia wa Gabon.

Chelsea ilionekana kutawala kipindi cha pili lakini shambulizi la kustukiza lililofanywa na washika mitutu hao wa London dakika ya 67, lilizaa matunda kwa Aubameyang   kuwafungia bao la pili na ushindi.

Licha ya wachezaji wa Chelsea kuandamwa na majeraha kwenye mchezo huo, walijikuta wakimaliza pungufu baada ya kiungo wao, Mateo Kovačić kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na mwamuzi, Anthony Taylor iliyofuatiwa na nyekundu baada ya kucheza rafu.