Ataiweza? Ukubwa wa jezi Namba 7 aliyokabidhiwa Cavani Man United

MANCHESTER, ENGLAND. MANCHESTER United imethibitisha kwamba Edinson Cavani atavaa jezi Namba 7 kwenye kikosi hicho.

Straika Cavani alinaswa kwa uhamisho wa bure baada ya kuachwa na Paris Saint-Germain mwishoni mwa msimu uliopita na amesaini miaka miwili huko Old Trafford.

Na klabu imethibitisha kwamba atavaa jezi Namba 7 yenye hadhi kubwa klabuni hapo, akipewa mtihani mkubwa wa mastaa George Best, Eric Cantona, David Beckham na Cristiano Ronaldo waliotamba na jezi hiyo. Wachezaji wengine waliofuatia kwa kuvaa jezi Namba 7 na kuchemsha kwelikweli ni pamoja na Alexis Sanchez, Memphis Depay, Angel Di Maria na Michael Owen.

Hii hapa orodha ya mastaa waliowahi kuvaa jezi Namba 7 kwenye kikosi hicho cha Man United na kile walichofanya kabla ya Cavani kupewa uzi wenye namba hiyo yenye thamani kubwa huko Old Trafford.

GEORGE BEST, 1963-74

Mechi — 474

Mabao — 181

Katika zama ambazo namba za jezi zilikuwa sio muhimu kumilikiwa na mchezaji mmoja, staa George Best alivaa Namba 7 katika mechi 141 kati ya 474 alizoitumikia Man United. Mwaka 1966, Best alivaa jezi hiyo na hakika kiwango chake cha uwanjani kilikuwa balaa kubwa, akifunga mabao muhimu kwenye mechi za fainali za michuano ya Ulaya, ikiwamo yale mabao yake mawili katika ushindi wa 5-1 dhidi ya Benfica huko Lisbon, Ureno. Best anahesabika na wengi kama mmoja wa wachezaji waliokuwa na kipaji kikubwa cha soka waliowahi kutokea Uingereza. Alishinda Ballon d’Or mwaka 1968 na alishinda namba tatu 1971.

BRYAN ROBSON — 1981-94

Mechi — 461

Mabao — 99

Alichukua jezi Namba 7, licha ya kwamba Steve Coppell bado alikuwa kwenye kikosi hicho. ‘Captain Marvel’ alikuwa na bahati mbaya kuichezea Man United iliyokosa ubora wa kuwania mataji kwenye miaka ya 1980 na hakika, ndiye aliyekuwa nahodha wa muda mrefu zaidi katika timu hiyo, huku akiichezea England pia mara 90. Alikuwa kiongozi wa wenzake ndani ya uwanjani na mabao yake mawili yaliisaidia Man United kupindua matokeo ya kuchapwa 2-0 na Barcelona kwenye michuano ya Ulaya na kushinda kibabe katika usiku wa soka matata kabisa huko Old Trafford mwaka 1984. Alishinda ubingwa wa ligi mara mbili, Kombe la FA mara nne, Kombe la Ligi na Kombe la Washindi Ulaya.

ERIC CANTONA — 1992-97

Mechi — 185

Mabao — 93

Mchezaji wa kwanza kusainishwa rasmi kwenye Namba 7 alikuwa staa wa Ufaransa, Eric Cantona. Staa huyo alikuwa na mchango mkubwa sana kwenye kikosi hicho na kuibadili Man United kuwa timu ya kibingwa kwenye Ligi Kuu England. Akiwa Man United alishinda mataji manne ya ligi katika misimu mitano na msimu ambao alishindwa kunyakua ubingwa ni ule ambao alifungiwa kwa miezi minane kutokana na kumrukia daruga la kung-fu kicking shabiki wa Crystal Palace, aliyekuwa akitoa maneno ya dhihaki dhidi yake katika moja ya mechi zao. Akiwa na jezi hiyo, Cantona alishinda namba tatu kwenye Ballon d’Or mwaka 1993.

DAVID BECKHAM — 1992-03

Mechi — 394

Mabao — 85

Mataji sita ya Ligi Kuu England, mawili ya Kombe la FA, Ligi ya Mabingwa Ulaya mara moja na mataji mengine, huku akishinda namba mbili kwenye Ballon d’Or mwaka 1999. Staa Beckham aliibukia kutoka kwenye akademia ya Man United na mwanzo alikuwa akivaa jezi Namba 28, kisha ikaja Namba 24, Namba 10 na hatimaye akakabidhiwa Namba 7 baada ya Cantona kuondoka. Mchango wa Beckham akiwa na jezi Namba 7 mgongoni ulikuwa mkubwa sana ukiwamo asisti zake muhimu kwenye robo fainali, nusu fainali na fainali yenyewe ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 1999, ambapo miamba hiyo ya Old Trafford ilibeba mataji matatu makubwa msimu huo. Aliondoka kwenda zake Real Madrid mwaka 2003.

CRISTIANO RONALDO — 2003-09

Mechi — 292

Mabao — 118

Kwenye kikosi cha Man United, staa Cristiano Ronaldo akiwa na jezi namba 7 mgongoni, alishinda mataji matatu ya Ligi Kuu England, Kombe la FA, Kombe la Ligi, Ligi ya Mabingw Ulaya, Klabu Bingwa Dunia na alishinda Ballon d’Or. Mambo yake yalikuwa makali balaa ndani ya uwanja na kuitendea haki kabisa namba hiyo, ambayo alikabidhiwa kutoka kwa David Beckham. Ronaldo alitua Man United akiwa na umri wa miaka 18 tu na kocha Sir Alex Ferguson hakuona tatizo kumkabidhi jezi hiyo yenye heshima kubwa huko Old Trafford.

MICHAEL OWEN — 2009-12

Mechi — 52

Mabao — 17

Supastaa Mwingereza, Michael Owen baada ya kunaswa na Manchester United alikabidhiwa jezi Namba 7, wakati huo Cristiano Ronaldo akiwa ndio kwanza ameondoka kwenye timu hiyo kwenda Real Madrid. Kipindi hicho, Owen alikuwa anakaribia miaka 30 na alikuwa ameachwa na timu iliyokuwa imeshuka daraja, Newcastle United na alisajiliwa na Man United kwa sababu tu walifeli kwenye mpango wao wa kumsajili Karim Benzema. Lakini, akiwa namba 7, kitu ambacho kinakumbukwa kuhusu Owen ni lile bao lake la dakika za mwisho dhidi ya Manchester City na lile la fainali ya Kombe la Ligi na hat-trick yake kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

ANTONIO VALENCIA — 2009-19

Appearances — 339

Mabao — 25

Staa, Antonio Valencia alinaswa na Man United mwaka 2009 akitokea Wigan Athletic. Valencia alitamba sana Old Trafford akiwa na jezi Namba 25 mgongoni. Badaa ya misimu mitatu ya kutamba na jezi hiyo, akicheza kiwango matata kabisa, Valencia alikabidhiwa jezi Namba 7 katika msimu wa 2012-13. Na baada ya msimu huo kumalizika, ambapo Man United ilibeba ubingwa wa ligi, Valencia aliomba kurudishiwa jezi yake ya zamani, Namba 25. Akiwa kwenye kikosi hicho, Valencia alibeba ubingwa wa Ligi Kuu England mara mbili, Kombe la FA na Europa League.

ANGEL DI MARIA — 2014-15

Mechi — 32

Mabao — 4

Huu ulikuwa usajili wa rekodi kwa Man United na England kwa kipindi hicho, wakati Muargentina huyo aliponaswa kwa ada ya Pauni 59.1 milioni.

Di Maria alitua Old Trafford akitokea Real Madrid, mahali ambako alikuwa kwenye kiwango bora kabisa ikiwamo shoo ya maana kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na hapo Man United ilionekana imefanya usajili matata. Lakini, kiwango chake kiliporomoka kwa kasi sana na akawa mzigo tu kwenye timu na kuwafanya Man United kumuuza baada ya msimu mmoja tu kwa ada ya Pauni 44 milioni.

MEMPHIS DEPAY — 2015-16

Mechi — 53

Mabao — 7

Memphis alikabidhiwa jezi Namba 7 baada ya kutua tu kwenye kikosi cha Man United aliposajiliwa na Mdachi mwenzake, Louis van Gaal kutoka PSV kwa ada ya Pauni 25 milioni. Alipokuwa PSV, Depay alikuwa bonge la mchezaji, lakini alipotua Man United na kupewa jezi hiyo ngumu kila kitu kilibadilika na kuwa mchezaji wa kawaida sana. Baada ya msimu mmoja tu, Depay alitolewa kwa mkopo kwenda Lyon kabla ya kuuzwa jumla. Akiwa Ufaransa kwenye kikosi cha Lyon, Mdachi huyo alirudi kwenye kiwango bora cha soka lake, akifunga mabao 53 katika mechi 134 na kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi lililofungwa Jumatatu iliyopita, alikuwa kwenye rada za Barcelona.

ALEXIS SANCHEZ — 2018-2020

Mechi — 45

Mabao — 5

Baada ya misimu minne ya kutamba akiwa na Arsenal, staa wa Chile, Alexis Sanchez aliamua kwenda kujiunga na Man United kwa ada iliyothaminishwa kuwa na thamani ya Pauni 32 milioni, kwa sababu lilikuwa ni dili la kubadilishana na mchezaji Henrikh Mkhitaryan. Robin Van Persie alimwonyesha Sanchez kwamba suala la mchezaji wa Arsenal kwenda Man United si tatizo, lakini yeye alipofanya hivyo mambo hayakuwa mambo kabisa. Aliishia kufunga mabao matano tu katika mechi 45 na kujikuta akitolewa kwa mkopo kwenda Inter Milan kabla ya kuruhusiwa aende moja kwa moja kujiunga na Wataliano hao bure kabisa.