Arsenal kazi mnayo, Vardy ndo kaja hivyo!

LONDON, ENGLAND. ARSENAL mpo? Hii inaitwa usiyempenda kaja.

Kwenye Ligi Kuu England, Arsenal itakuwa Emirates kuwakaribisha Leicester City. Kwenye kikosi cha Leicester City kuna mtu anaitwa Jamie Vardy - yeye ni balaa zito anapokabiliana na timu za Big Six kwenye Ligi Kuu England.

Straika Vardy ni kama amezikodi timu za Big Six kwenye Ligi Kuu England kutokana na namna anavyozifunga - akifunga mara nyingi kuliko mchezaji yeyote ndani ya miaka mitatu iliyopita.

Kwenye mechi 34 za ligi alizocheza dhidi ya Arsenal, Chelsea, Liverpool, Manchester City, Manchester United na Tottenham, Vardy amefunga mabao 21. Mwezi uliopita aliwapiga hat-trick Man City, Leicester City iliposhinda 5-2. Amekuwa hatari pia anapocheza dhidi ya Arsenal, akifunga mara saba katika mechi sita za mwisho alizocheza na wababe hao wa London Kaskazini. Jambo hilo linatuma meseji ya vitisho kwa mabeki wa The Gunners inayonolewa na Mikel Arteta, kwamba usiyempenda kaja.

Mastaa wengine matata kwa kufunga mara nyingi dhidi ya timu za Big Six kwenye Ligi Kuu England ni Danny Ings, ambaye kwenye mechi 18 amefunga mara 11, huku Sergio Aguero akifunga idadi kama hiyo mara 11 kwenye mechi 23.

Straika Harry Kane amefunga mara 12 kwenye mechi 26, wakati Mohamed Salah amefunga mabao 14 katika mechi 31 na Marcus Rashford amefunga mara 10 katika mechi 24.

Roberto Firmino amefunga mara 12 kwenye mechi 31, Raheem Sterling amefunga mara 11 katika mechi 29 na Kevin De Bruyne amefunga mabao tisa katika mechi 24 za Big Six sawa na Anthony Martial, ambaye pia amefunga mara tisa katika mechi 24 alizokabiliana na wababe hao wa Big Six kwenye Ligi Kuu England.

Mechi nyingine za Ligi Kuu England zitakazopigwa leo Jumapili, Southampton watakuwa nyumbani kuwakaribisha Everton, ambao wapo kwelikweli kwenye ligi hiyo msimu huu, wakati Wolves wao watakuwa na shughuli nzito mbele ya Newcastle United. Kesho, Jumatatu, Brighton watacheza na West Brom, wakati Burnley watamkaribisha Jose Mourinho na chama lake la Spurs huko Turf Moor ambapo mwamuzi atakuwa Michael Oliver.