Ambundo atamani ufungaji bora

Muktasari:

  • Ambundo aliyewahi kuchezea Mbao FC, aliibuka Mchezaji Bora wa Ligi Kuu Januari na kuchukua kitita cha Sh1 milioni

Dar es Salaam. Nyota wa Alliance FC, Dickson Ambundo amefichua ndoto yake ni kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Ambundo aliyejiunga na Alliance miaka miwili iliyopita akitokea Mbao FC hadi sasa amefunga jumla ya mabao tisa katika Ligi Kuu na hivi karibuni alinyakua tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu mwezi Januari.

Mshambuliaji huyo amesema kuwa tuzo hiyo imempa hamu ya kufanya mambo makubwa zaidi hasa kupata tuzo ya ufungaji bora msimu huu.

"Kiukweli nafasi niliyoipata ya kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Januari ni kubwa na imenipa motisha ya kuongeza juhudi. Kikubwa natakiwa nipambane ili niwe Mfungaji Bora," alisema Ambundo.

Mshambuliaji huyo alisema uelewano mzuri wa kitimu ndio siri inayopelekea awe anafunga mara kwa mara msimu huu.