Alliance yamtema Mnyarwanda, Makata aula

Thursday August 9 2018

 

By Masoud Masasi

Mwanza. Klabu ya Alliance FC imemtangaza Mbwana Makata kuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, na kuweka wazi kuachana na Baptiste Kayiranga aliyekuwa ameletwa kikosini hapo kutoka Nchini Rwanda.

Kocha Kayiranga alitua nchini Mei 26 na kusaini kandarasi ya miaka miwili, ambapo alikaa kwa takribani mwezi mmoja kisha kuondoka kimya kimya nchini kwao kwa wito maalumu wa kuinoa timu yao ya Taifa ya Wanawake.

Akizungumza Jijini hapa, Katibu Msaidizi wa timu hiyo, Hassan Kasembe alisema kuwa kuanzia sasa Alliance itakuwa chini ya Kocha Mbwana Makata akisaidiwa na Kessy Mzirai na Renatus Shija.

Alisema kuwa awali walimleta kocha Mnyarwanda Kayiranga, lakini cha kushangaza aliondoka bila kuaga na kuwapa wakati mgumu kusaka mwalimu mpya.

“Kulikuwepo na sintofahamu juu ya Kocha Kayiranga kuwepo au kutokuwepo Alliance, naomba niseme wazi kuwa tumeachana naye baada ya kukiuka masharti ya mkataba na kuanzia sasa majukumu yatakuwa chini ya Makata,” alisema Kasembe.

Katibu huyo aliongeza kuwa timu hiyo inaendelea kujiandaa vyema kuelekea msimu ujao na kwamba wanaridhishwa na mwenendo wake na wanaamini watafanya vizuri.

 

Advertisement