Alliance yamtema Javu

Muktasari:

Budodi aliongeza kuwa timu inatarajia kuingia kambini mwishoni mwa mwezi huu ambapo watakuwa wamekamilisha zoezi la usajili tayari kwa maandalizi ya msimu mpya.

MWANZA.KLABU ya Alliance imewatema nyota wake sita akiwamo straika wake mkongwe Hussein Javu kupisha sura mpya kwa ajili msimu ujao wa Ligi Kuu.

Baada ya kuwatema wachezaji hao, tayari wachezaji watatu wamepata timu zingine ambao ni Bigirimana Blaise (Namungo FC), Mapinduzi Balama (Yanga) na Kipa Ibrahim Isihaka aliyejiunga na Gwambina FC ya Daraja la Kwanza.

Wengine mbali na hao ni Paul Maona na Songa Gerard ambao imeelezwa kutemwa kupisha usajili mpya.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Klabu hiyo, Yusuph Budodi alisema wamefikia maamuzia hayo ili kutowapotezea muda kwani ni vijana wanaohitaji kucheza hasa timu zingine.

Alisema watasajili wachezaji wengine wakiwemo wa kigeni, hivyo wasio na nafasi ndani ya timu yao wameachana nao mapema ili wawe na nafasi ya kusaka timu.

“Kuna ambao wamepata timu, lakini kama Maona amekuwa na majeruhi ya muda mrefu hivyo tumeamua tuachane naye, tunajipanga kuleta nyota wapya ambao wana uwezo mkubwa,” alisema Budodi.

Budodi aliongeza kuwa timu inatarajia kuingia kambini mwishoni mwa mwezi huu ambapo watakuwa wamekamilisha zoezi la usajili tayari kwa maandalizi ya msimu mpya.

“Kufikia Juni 30 kila kitu kitakuwa kimekamilika kwa upande wa usajili sehemu zote na tayari kuingia kambini, tunaendelea kukamilisha mazungumzo ya mwisho na tunaowahitaji”alisema Budodi.