Aliyemsajili Kompany afunguka ilivyokuwa

Muktasari:

Bosi huyo wa zamani wa Kompany alisema, wakati mpira uliopigwa na beki huyo ukienda kutinga wavuni, alisimama na kushangilia kama mtoto.

MANCHESTER, ENGLAND.VINCENT Kompany Jumatatu iliyopita alipokea meseji kwenye simu yake kutoka kwa mtu ambaye ndiye aliyemsajili kuja Manchester City miaka ile ya tabu kabla ya ujio wa Sheikh Mansour klabuni hapo.

Mtu huyo, aliyekuwa kocha msaidizi wa Man City wakati huo,Mark Bowen amekuwa akiwasiliana na Kompany tangu mwaka 2009 alipoondoka kwenye timu hiyo na bosi wake, Mark Hughes.

Bowen anasema muda mfupi tu baada ya Kompany kufunga bao muhimu dhidi ya Leicester City zilizoweka hai mbio zao za ubingwa wa Ligi Kuu England, alinyanyua simu yake na kutuma meseji kwa beki huyo matata huko Etihad.

Bowen anasema meseji yake aliyomwaandikia Kompany ilisomeka hivi: ‘Dakika 71 zimepita, Manchester City inahitaji maajabu. Anasimama kapteni na kufanya maajabu’.

Bosi huyo wa zamani wa Kompany alisema, wakati mpira uliopigwa na beki huyo ukienda kutinga wavuni, alisimama na kushangilia kama mtoto.

“Mpira ulipokuwa ukielekea wavuni, nilisimama kushangilia. Licha ya kile tulichofanyiwa mimi na Mark, lakini huwezi kupoteza hisia na timu ambayo iliwahi kukuajiri. Ni kitu kizuri pia kuona wanabeba ubingwa kupitia mtu ambaye ulimsajili wewe kwenye timu,” alisema Bowen.

Akirudi nyuma hadi Agosti 2008, kipindi hicho Man City ilipokuwa chini ya umiliki wa Thaksin Shinawatra, mambo yalikuwa magumu kuliko starehe wanayopata siku hizi.

Bowen anasema wakati wakiwa na wiki chache tu kwenye timu yeye na kocha Mark Hughes waliambiwa wauze wachezaji haraka, kwa sababu timu ilikuwa inahitaji pesa.

“Sisi hatukutaka kuuza kwa sababu timu ingekuwa dhaifu. Lakini, tuligundua tayari walikuwa wameshakubaliana dili ya kumuuza Vedran Corluka kwenda Tottenham. Mark aliwaambia atakubali kupitisha hilo kama wataletwa wachezaji wengine wawili au mmoja.

“Wachezaji hao wawili walipokuwa Pablo Zabaleta na Vinny Kompany,” alisema.

Zabaleta aliigharimu Man City Pauni 6.45 milioni kutoka Espanyol na kwenye kikosi hicho alicheza zaidi ya mechi 300, akibeba mataji matatu ya Ligi Kuu England, Kombe la Ligi mara tatu na Kombe la FA. Kompany alinaswa kutoka Hamburg ya Ujerumani kwa ada ya Pauni 6 milioni.

Kipindi hicho Man City ilikuwa timu ya kuuza wachezaji, lakini Hughes alipambana vikali kumsajili Kompany.

Bowen alisema baada ya Kompany kutua kwenye timu hiyo walimwambia wamemsajili kwa sababu wanataka kufanikiwa, kitu ambacho walimwambia kipindi hicho kabla hata Sheikh Mansour hajafika hapo kuchukua timu.

“Tulianza kumchezesha kwenye beki, lakini yeye kila siku alikuwa anapiga hodi ofisini kwa Mark akitaka acheze shwe kwenye kiungo ya kati. Mark alim wam bia kwamba anam tazama kuwa nahodha makini wa baadaye akicheza kwenye safu ya mabeki,” alisema Bowen. Na tangu hapo, Kompany amekuwa mchezaji muhimu kwenye safu ya ulinzi ya Man City kwa karibu miaka 11.

“Nilimtumia meseji na tumekuwa tukizungumza mengi tu, unajua kile kilichotukuta sisi pale na mafanikio yake anayopata ni jambo zuri. Kizuri ni kwamba ameendelea kuwa mtu wa aina ileile tangu tulipomsajili.

“Bado amebaki kuwa vilevile, sio mtu wa majigambo. Wangekuwa watu wengine kwa mafanikio aliyopata, basi angebadilika kitabia, amebaki kuwa vilevile kama alivyokuwa mwanzoni.