Algeria, Senegal zamuibua Amunike

Tuesday July 16 2019

 

By Imani Makongoro

Dar es Salaam.Wakati Senegal na Algeria zikifuzu fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon), mchezo huo umehusishwa na aliyekuwa Kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilisitisha kibarua cha Amunike siku chache baada ya Taifa Stars kurejea ikitokea Misri ilikoshiriki Fainali za Afcon.

Matokeo ya Taifa Stars kufungwa mabao 2-0 na Senegal kabla ya kulala 3-0 ilipocheza na Algeria, yanatajwa ni miongoni mwa sababu zilizochangia kumng’oa Amunike. Pia ilifungwa 3-2 na Kenya.

Rekodi ya Algeria iliyofuzu fainali bila kufungwa na Senegal iliyopoteza mchezo mmoja dhidi ya Algeria, imewaibua wadau wa soka ambao wametoa maoni tofauti.

Miongoni mwa wadau hao ni nahodha wa zamani wa Yanga, Ally Mayay aliyesema kitendo cha timu hizo kucheza fainali kinathibitisha ubora wa vikosi hivyo na Amunike hakustahili kutimuliwa.

Akizungumza jana, Mayay alisema Amunike alitwishwa mzigo asiostahili kuubeba kwa kuwa rekodi ya Algeria na Senegal ni tishio katika soka la Afrika.

Advertisement

“Tanzania tulikwenda Misri ili kuzoea mashindano, katika kundi letu timu ambayo tulionekana tunaweza kupambana nayo ni Kenya na tulifanikiwa, tulianza kuwafunga na wao wakasawazisha na kuongeza bao, lakini si Algeria wala Senegal na matokeo yameonekana,” alisema Mayay.

Kocha Kenny Mwaisabula alisema uwezo wa Senegal na Algeria ni mkubwa na hauwezi kulinganishwa na Taifa Stars.

“Niliwahi kusema Amunike alitolewa kimakosa, kiufundi amefanya kazi yake ipasavyo na kwa matokeo ya Algeria na Senegal ni ishara kocha alionewa,” alisema.

Kocha Fred Felix ‘Minziro’ alisema, “kuhusu Amunike uamuzi ulishafanyika siwezi kuingilia, lakini matokeo ya Algeria na Senegal yanaashiria tukifanya maandalizi mazuri tutafanya kitu kwenye Afcon ya mwaka 2021.”

Advertisement