Ajibu ni zaidi ya thamani ya dola

Tuesday June 11 2019

 

By Nicasius Agwanda

Dar es Salaam. Siku moja na itakuwa asubuhi na wengi tutakuwa kwenye vibanda vya magazeti, vijiwe vya kahawa pia maeneo ya kukutania tukijadili bao zuri  linaloweza kuwa bora zaidi msimu huo likiwa limetoka kwenye mguu wa kijana wa Kitanzania.

Litakuwa bao lililofungwa katika moja ya mechi ya ligi kubwa duniani, litakuwa bao la kipekee lenye thamani na bao ambalo litabeba bendera yetu vyema kutokana na umuhimu wake.

Natamani liwe bao la Mbwana Samatta msimu ujao, natamani liwe bao la Saimon Msuva kama taarifa zake za kuondoka kwenda Ulaya ni za kweli au natamani liwe bao ambalo litamaanisha Shabaani Chilunda au Farid Mussa wamejiongezea thamani na wanauzwa bei ghali.

Hizi ni fikra za matamanio ambazo Watanzania wengi tunatamani kushuhudia kabla pumzi zetu hazijaondoka. Hii ni hamu ambayo tunaamini ikitimia basi AFCON kwetu itakuwa sio suala gumu na hiki ni kitu ambacho tunaamini iwapo kikitokea kitabadili fikra za vijana wengi ambao hawafahamu namna gani wanapaswa kuishi kwenye tasnia ya michezo.

Dunia imekuwa katika mabadiliko makubwa ya Kiteknolojia na ugunduzi wa kila siku ambao unafanya maisha yarahisishwe katika nyanja nyingi za utendaji kazi, hivyo kuwa katika ulimwengu mpya kabisa wa kila jambo.

Dunia haina siri tena na haihitaji akili nyingi kupindukia kufanya baadhi ya mambo. Siku hizi hata mawasiliano yamekuwa si tena suala la kutegemea nyenzo moja ambayo ni simu za kawaida bali mitandao ya kijamii imeingilia kati suala hili.

Advertisement

Wakati huo dunia ikiwa inaendelea kukimbia kwa kasi, bado tumeamua kuvaa gamba la kobe hapa Tanzania, tunaamini taratibu ndio mwendo na pia haraka haraka haina baraka.

Upande mwingine dunia ikiwa imetawaliwa na teknolojia michezo kwa sasa, sisi bado tupo analojia ya uendeshaji soka na pia wakati kukiwa na kila aina ya nafasi huko nje wapo wanaoamini hawawezi kutoka nje ya noti ya Tanzania, hawana hamu na dola za Marekani. Hivi karibuni zilisambaa taarifa za mchezaji Ibrahim Ajibu kutakiwa na TP Mazembe kabla ya taarifa nyingine kusema kuwa “dili” limekufa kwa sababu TP Mazembe na Ajibu walishindwa kuafikiana juu ya maslahi binafsi.

Sitaki kuingia ndani katika maslahi binafsi ya Ajibu, kiuhalisia sikushituka kwa sababu nilikuwa nasubiri Ajibu anishangaze kwa kuamua kwenda TP Mazembe.

Pamoja na kutokushtuka kwangu, bado moyo wangu umesononeka kwa sababu bado Taifa linaangamia kimichezo kwa kukosa watu sahihi wa kusimamia maslahi ya muda mrefu ya wachezaji.

Ajibu anaweza kupewa mshahara mkubwa kwa fedha za Tanzania kuliko dola za TP Mazembe, lakini kuna jambo kubwa zaidi ambalo halipo kwenye medula za wachezaji ambalo Watanzania tunatamani.

Ajibu akiwa TP Mazembe ana uhakika wa kuwa mgombea Ubingwa wa Afrika. Ajibu anapotua Mazembe anakua na uhakika iwapo atacheza vyema atakuwa ametengeneza “CV” imara ambayo itamfanya kula vyema hata wakati wa pensheni yake. Maisha ya sasa ya Thomas Ulimwengu. Wakati wengi tukiamini si yule tena, klabu kubwa bado zinamfuata kwa sababu zinaamini ni mchezaji bora kwa sababu tu alicheza TP Mazembe. Huyu ataendelea kuzurura katika klabu kubwa na mpaka arejee Azam au Simba atakuwa amebakiza msimu mmoja kustaafu.

Unapokuwa unaenda nje ya nchi sio tu kuwa unajipa changamoto ya kutamani kusogea mbali zaidi bali pia unajipa thamani ya kuwa mchezaji ghali na pia inabadili kabisa namna yako ya kufikiri maisha yako ya soka na inakuongezea wigo mpana wa kujifunza kutoka kwa waliokuwa bora zaidi na kingine ni kile ambacho wengi wanakiita “exposure.”

Inawezekana tafsiri ya kucheza nje bado haijaeleweka kwa wengi na pengine hata washauri wa hawa wachezaji nao wanaamini maslahi ya kucheza nje yanaanzia kwenye mshahara mkubwa kuliko Tanzania.

Usishangae Ajibu akawa ni mhanga wa fikra hizi pia. Umefika wakati wachezaji hawa wafahamu kuwa tunapotaka watoke nje ni zaidi tu ya thamani ya dola, ni zaidi ya magari watakayonunua. 

Kikubwa ni mafunzo, kutangaza Taifa, kufungua njia kwa wengi, kuacha jina linalosimama kwenye kumbukumbu na kingine ni kujiongezea changamoto zaidi.

Kama haitoshi huwezi kuwa mfalme wa Simba au Yanga halafu ukawa mfalme nje ya nchi, lakini tambua kuwa unaweza kuwa mfalme klabu za nje kama TP Mazembe halafu ukawa mfalme wa Watanzania kwa wakati huohuo bila kujali itikadi za klabu. Samatta anaweza kusimulia hili na hata Msuva kaanza kuonja ufalme wa Watanzania.

Advertisement