Ajibu arudishwa kitemi Simba

Muktasari:

Ajibu alijiunga na Simba kabla ya msimu huu kuanza akitokea Yanga ambako alicheza kwa misimu miwili tangu alipojiunga nao mwaka 2017 akitokea Simba.

MSHAMBULIAJI wa Simba, Ibrahim Ajibu amerudishwa katika kambi ya timu hiyo na leo Jumatatu  alikuwa katika mazoezi ya kikosi hicho yaliyofanyika leo saa 11.00 jioni katika uwanja wa Mo Simba Arena, Bunju jijini Dar es Salaam.

Ajibu alifukuzwa kambini na kocha mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck kwa kosa la kuchelewa kufika kambini.

Adhabu hiyo ambayo Ajibu alikutana nayo si kufukuzwa kambini pekee yake bali alitozwa faini ya Sh 200000 ambayo atakatwa katika mshahara wake mwisho wa mwezi Mai.

Jana Jumatatu asubuhi Ajibu alifika kambini kwa Simba, Mbweni kisha akawa na mazungumzo mafupi na Vandenbroeck  na baadaye aliruhusiwa  kuwa miongoni mwa  wachezaji ambao watafanya mazoezi jioni.

Katika mazoezi hayo Ajibu alikutana na cha moto kwani alikuwa akikimbizwa mbio za kuzunguka uwanja huku Sven akiwa anamsimamia.

Wakati Ajibu akiwa anakimbia mbio za kasi na pole pole akizunguka uwanja, Sven alikuwa akimsimamia huku wachezaji wengine wote wakiwa kati kati ya uwanja  wakifanya mazoezi ya kawaida.

Mazoezi hayo ya kawaida kwa wachezaji wengine yalikuwa yakisimamiwa na kocha wa viungo, Adel Zrane aliyekuwa sambamba na kocha msaidizi Selemani Matola.

Ajibu hakuwa anakimbia mwenyewe bali alikuwa na wachezaji wengine, Rashid Juma na Francis Kahata ambaye nae ndio alikuwa anafanya mazoezi ya kwanza yale ya uwanjani akiwa na kikosi hiko tangu aliporejea nchini.

Sven alionekana kumkazania  Ajibu akimtaka akimbie kwa kasi kama vile ambavyo alikuwa.