Aiyee awatoka Makambo, Kagere

Muktasari:

  • Pia alizungumzia kitendo cha kutoitwa kwenye timu ya Taifa Stars chini ya kocha Emmanuel Amunike kwamba halimsumbui kwa sababu malengo yake makuu ni kiatu cha dhahabu.


SALIM Aiyee wa Mwadui FC, anaendelea kuwaacha mbali mastaa Heritier Makambo (Yanga) na Meddie Kagere (Simba) baada ya kufikisha idadi ya mabao 15 kwenye msimamo wa wafungaji.

Aiyee aliliambia Mwanaspoti kwamba katika mechi zilizobakia anatamani kufunga mabao yasiopungua nane,anayoamini yatamweka kwenye mazingira mazuri kwenye msimamo wa wafungaji.

Alimtaja straika anayempasua kichwa na kuona anaweza akapindua meza kuwa ni Meddie Kagere wa Simba, akitoa sababu kwamba bado wana mechi nyingi na kwamba ni mchezaji anayelijua goli.

“Simba bado wana mechi nyingi na aina ya uchezaji wa Kagere ni ule wa upambanaji kiasi kwamba ninaamini atafunga mabao mengi ndio maana natamani nifunge kwenye mechi zilizosalia yesiwe chini ya nane.

“Kadri ninavyofunga ari ya kutamani kuwa na mabao mengi inaongezeka, lakini pia huo ni ushirikiano wa timu nzima kwa namna ambavyo wanajua kunitengenezea nafasi zinazofanya niongoze kwa mabao 15 kwa sasa,”alisema.

Pia alizungumzia kitendo cha kutoitwa kwenye timu ya Taifa Stars chini ya kocha Emmanuel Amunike kwamba halimsumbui kwa sababu malengo yake makuu ni kiatu cha dhahabu.

“Siwazi chochote kutoitwa timu ya Taifa, muda ukifika nitaichezea hata hivyo msimu huu tangu unaanza nilikuwa natamani kuwa kwenye rekodi ya watu wanafunga mabao mengi.”