Aisee! Mbappe mambo yazidi kumnyokea

Thursday April 25 2019

 

By Thomas Ng'itu

WAKATI ofa zikiwa zinazidi kumiminika kwa mshambuliaji kelvin John ‘Mbappe’ wa Timu ya Taifa Tanzania chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, mwenyewe amesema kwa upande wake ni jambo la kheri.

Kelvin ambaye amekuwa na kiwango bora anapokuwa uwanjani akiitumikia Timu ya Serengeti Boys, anahusishwa kutakiwa na klabu za Monaco, Manchester City, Lille pamoja na Ajax ya Uholanzi.

Mwanaspoti lilimtafuta mchezaji huyo ambapo alikiri kuwepo na ofa hizo huku akisema yeye yupo tayari kufanya kazi katika timu yoyote ile ambayo itafikiana makubaliano na msimamizi wake.

“Kweli kuna ofa za Monaco, Lille, Manchester City, Monaco na Ajax lakini mimi nipo tayari kufanya kazi popote kwasababu mimi ni mchezaji mdogo natafuta maisha bado na nina ndoto ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi,” alisema.

Akizungumzia fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 (AFCON U17) Serengeti Boys ilishika mkia baada ya kupoteza mechi zote tatu dhidi ya Nigeria, Uganda na Angola, alisema amejiongezea uzoefu kiasi cha kujiona amezidi kuimarika.

“Mashindano yalikuwa mazuri, binafsi nimejifunza vitu vingi hasa baada ya kukutana na mabeki ambao wanacheza Ligi mbalimbali, kikubwa najiona kabisa kwamba nimeongezeka katika uchezaji wangu,” alisema.

Advertisement

Katika mashindano hayo ambayo mechi za nusu fainali zilichezwa jana Jumatano, Kelvin alionyesha umahiri mkubwa katika kupambana na mabeki wa timu pinzani kiasi cha kuwavutia mawakala na wasaka vipaji wanaoyafuatilia.

Advertisement