African Lyon iwe funzo kwa timu zingine

Wednesday May 15 2019

 

By Mhariri

LIGI Kuu Bara imesaliwa na mechi za raundi zisizozidi tatu kabla ya kumalizika kwa msimu wa 2018-2019, huku African Lyon ikiwa klabu ya kwanza kushuka daraja.

Lyon iliyorejea Ligi Kuu msimu huu imerudi ilipotoka baada ya juzi kuchapwa mabao 3-2 na Mbao FC kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Kipigo hicho kimeifanya klabu hiyo kusaliwa na alama zao 22 baada ya kucheza mechi 34 na kama itamaliza michezo yake minne iliyosalia na kushinda zote itafikisha pointi 34 ambazo zimeshapitwa na klabu nyingine 19 zinazoshiriki ligi ya msimu huu. Klabu hiyo yenye maskani yake Temeke, imeshinda michezo minne tu kati ya iliyochezwa huku ikiambulia sare 10 na vipig0 20 ikiweka rekodi ya timu iliyochemsha vibaya msimu huu, tofauti na ilivyotarajiwa wakati ilipoanza msimu. Ndiyo timu iliyofunga idadi ndogo ya mabao katika Ligi Kuu ya msimu huu kulinganisha na klabu nyingine 19, huku ikiwa ni timu ya pili iliyoruhusu mabao mengi ikizidiwa na Mwadui iliyofungwa 48 wakati Lyon ikifungwa 46.

Baadhi ya wadau wa soka walishaibarishia mapema timu hiyo kurudi ilipotoka hata kabla ya kuanza kwa msimu kutokana na kuwa na rekodi ya kupambana kupanda Ligi Kuu, lakini ikiwa haina juhudi za kuifanya idumu kwa muda mrefu katika ligi hiyo.

Rekodi zinaonyesha Lyon, ilipanda Ligi Kuu mara ya kwanza mwaka 2008 na kuicheza msimu wa 2008-2009 na kushuka 2012-13 kabla ya kurejea tena 2016-2017 na kurudi ilipotoka msimu huo huo.

Msimu uliopita baada ya kupambana sana, timu ilirejea tena kwa kishindo, lakini ndani ya msimu huu imejikuta ikishinda kuhimili vishindo na kushuka rasmi ikiwa timu ya kwanza, tena ligi ikisaliwa na michezo kadhaa kabla ya kufungwa kwa msimu.

Advertisement

Bila ya shaka Lyon inaacha somo kubwa kwa klabu zilizopanda Ligi Kuu ya msimu ujao, yaani Namungo FC na Polisi Tanzania ambao nao ni wazoefu wa kupanda na kushuka katika ligi hiyo kubwa kwa ngazi za klabu nchini. Lyon ni kama inazipa ishara klabu hizo na ile itakapopatikana kwenye playoff kwamba kama hazitajipanga vyema basi ni wazi zitakuja na kurudi Daraja la Kwanza kama ambavyo yenyewe imekumbana na kadhia hiyo. Lakini pia ni somo tosha kwa wamiliki wa klabu za Ligi Kuu kuwa, ligi hiyo si lelemama na lazima klabu ziandaliwe kwa malengo ya msimu mzima na zisiwe zinaendeshwa kwa mihemko ya muda mfupi tu.

Hatuna maana kwamba Lyon ilikuwa ikiendeshwa kwa mihemko, bali kwa jinsi ambavyo kwa muda mrefu imekuwa ikipanda na kuwa mikakati mingi ikiwamo kuleta makocha wa kigeni na hata nyota wa kigeni kabla ya kukimbizwa ni mambo yaliyoiangusha.

Inawezekana wamiliki wana kiu ya kuifanya Lyon iwe moja ya klabu ya kisasa na yenye kujumuisha wachezaji mchanganyiko kwa nia ya kutengeneza matokeo na kukimbizana na klabu kubwa, lakini kwa bahati mbaya mambo ya kiuchumi yanaikwaza.

Hata hivyo, kama wadau wa michezo na hasa soka, tunaamini Lyon bado ilikuwa inaweza kujengwa na kuundwa na nyota wazawa na hata kunolewa na kocha wa ndani, lakini ikajiwekea mipango mizuri kama inavyojiwekea inapotaka kupanda Ligi Kuu.

Kwa wanaofuatilia timu hiyo inapokuwa nje ya Ligi Kuu, huwa inatengenezewa vizuri na kuwa na mikakati mizuri na hatimaye hufanikiwa kupanda, lakini ndani ya muda mfupi huwa timu ya ovyo na kuchemsha kabla ya kurudi ilipotoka.

Tunalisema hili kwa kurejea rekodi yao ya kupanda na kushuka katika Ligi Kuu na hali ambayo imeikuta msimu huu ikikimbiwa na kocha kutoka Ufaransa sambamba na nyota kadhaa kwa sababu ya kushindwa kuwahudumia.

Hata wachezaji wazawa nao walitimka katika kikosi hicho kwa sababu mbalimbali ikiwamo kutolipwa na kujikuta wakirejea katika kutegemea wachezaji wa kawaida ambao wameshindwa kuipigania dakika za mwisho.

Hivyo, hata klabu zilizopanda na nyingine zinazoshiriki ligi lazima zijifunze kitu kupitia Lyon na harakati zake za ingia toka katika Ligi Kuu. Ni kweli Lyon siyo klabu ya kwanza kupanda na kushuka, African Sports, Manyema, Villa Squad, Vijana Ilala, Ashanti United na klabu nyingine zimewahi kukumbwa na adha kama hiyo, lakini klabu hiyo imekuwa ikitia fora kwa namna inavyotumia nguvu kubwa kupanda daraja na kushindwa kuitumia kuifanya idumu katika ligi hiyo. Bila ya shaka ikijiandaa kuicheza FDL ya msimu ujao, mabosi wa klabu hiyo watajifanyia tathmini na kuona wapi walipokuwa wanakosea na kurekebisha ili watakaporudi tena kama ni msimu wa 2021-2022 ama mbele ya safari wawe wamepata dawa.

Dawa itakayoifanya klabu hiyo irejee katika ligi hiyo ikiwa imejijenga kiushindani na pia iwe na uwezo wa kudumu kwa muda mrefu kwenye Ligi Kuu kwa muda mrefu kama baadhi ya timu ambazo zimekuwa zikidumu kwa misimu mingi hata kama zilishateleza.

Kwa sababu upo msemo kwamba fimbo ikuchapayo ndiyo ikufunzayo, hivyo ni wazi hii ingia toka kwa Lyon katika Ligi Kuu ni lazima iwe inajifunza kitu, kuwa kuna mahali labda wanakosea ndiyo maana hawana makazi ya kudumu katika Ligi Kuu kama wenzao.

Tuitakie tu kila la heri huko ilipoenda, lakini tukiiombea pia irejee kwa kishindo kama ilivyo desturi yao, kwani bado tunaamini ina nafasi yake katika Ligi Kuu Bara.

Advertisement