Adam: Simba na Mugalu wao tunawapiga

Thursday October 1 2020

 

By SADDAM SADICK

STRAIKA wa JKT Tanzania, Adam Adam amesema licha ya kasi waliyonayo Simba ikiwamo mastraika wao Chris Mugalu na mawinga wao Luis Miquissone na Clatous Chama lakini wasitarajie mteremko watakapokutana uwanjani Jumapili ya wiki hii.

Timu hizo zinatarajia kukutana Jumapili, ambapo JKT Tanzania itakuwa nyumbani ikikumbuka kupoteza mechi iliyopita dhidi ya Coastal Union bao 1-0, huku Simba wakitakata kwa mabao 3-0 mbele ya Gwambina.

Akizungumza na Mwanaspoti, Adam alisema wanawaheshimu Simba kutokana na ubora wao, lakini wasitarajie mteremko katika mchezo wao wa Jumapili kwani wamejipanga kubaki na ushindi.

Alisema licha ya kasi waliyoanza nayo haswa nyota wao, Mugalu, Luis na Chama lakini kwa jinsi JKT wanavyocheza kitimu, wapinzani hao wajiandae kisaikolojia kwani wanahitaji alama tatu. Hata hivyo, Luis na Chama huenda wasiwepo kikosi kwani wameitwa katika timu zao za taifa za Msumbiji na Zambia.

“Hatuwezi kuwaogopa au kuwadharau, hao sijui Chama, Mugalu, Kagere na Luis hawawezi kutuogopesha kwa sababu JKT tunacheza kitimu na tunahitaji pointi tatu ili kujiweka pazuri,” alisema Adam.

Straika huyo mwenye bao moja hadi sasa, aliongeza kuwa makosa waliyoyafanya katika mechi iliyopita na kusababisha kukosa matokeo mazuri, hawatarajii yajirudie kwenye mchezo ujao.

Advertisement

Alisema wachezaji wote wana ari na morali na kila mmoja anatamani kuona timu hiyo ikifanya vizuri na kutamba kuwa Simba lazima walale tena mapema.

Advertisement