Achana na VPL, Simba yaiwaza Stand

Friday February 21 2020

Achana na VPL, Simba yaiwaza Stand ,mechi ya Ligi Kuu Bara,Stand United,Kombe la Shirikisho Afrika,

 

By Charity James

WIKI ijayo, Simba itakuwa na kibarua cha kufukuzia tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Stand United huku leo Jumamosi akiwa na kibarua kingine cha mechi ya Ligi Kuu Bara.
Leo, Mabingwa hao watetezi watacheza na Biashara United saa 1 usiku uwanja wa Taifa ambapo mipango yao pia ni kutetea taji hilo na kupata nafasi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.
Hivi sasa, Simba wamesema hawataki kuacha kitu kwenye michuano hiyo miwili, huku wakijiapiza kwamba ni bora wakachukuwa mataji yote mawili, Ligi Kuu na KOmbe la FA ambapo baadaye watajua nini cha kufanya kwenye mataji hayo ingawa kiutaratibu itabidi taji la FA kama watachukuwa waligawe ama Shirikisho la Soka nchini (TFF) wataamua timu gani ipewe kuiwakilisha nchi kimataifa.
Simba walifuzu hatua ya 16 Bora ya kombe la FA baada ya kuifunga Mwadui FC bao 2-1huku Stand United yenyewe iliichapa Majimaji bao 2-1.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa amesema kuwa hawana mpango wa kuacha kitu na ndio maana wakimaliza mechi yao ya ligi watalazimika kutafuta usafairi wa haraka ambao hautawachosha wachezaji kwenda kuvaana na Stand United.
"Ni kuhakikisha kambi inakuwa na hali nzuri kwa kipindi hiki cha mashindano, maana tunataka kutetea ubingwa na kutwaa ubingwa wa FA, hivyo mipango yetu na benchi la ufundi inakwenda sambamba na viongozi. Maana hii ni moja ya mechi ngumu tunayoifuata ugenini.
"Tutasafiri na usafiri wa anga (Ndege) kwenda Shinyanga ambako tutacheza na Stand wiki ijayo Jumanne ambapo tutalazimika pia kurudi haraka kuja kucheza na KMC wiki hiyo hiyo ya Machi Mosi, hivyo ili wachezaji wasichoke ni kuwaandalia mazingira mazuri ya safari," alisema Senzo
Ukiachana na mechi ya FA, mechi zingine nne ikiwemo ya kesho Jumamosi, Simba watakuwa nyumbani dhidi ya KMC, Azam FC itakayochezwa Machi 4 na mechi ya watani itakayopigwa Machi 8 mwaka huu.

Advertisement