AFCON 2019 yala vichwa vya makocha

Muktasari:

  • Mwanaspoti linakuletea orodha ya makocha ambao tayari wameshatimuliwa na wale waliokalia kuti kavu kutokana na matokeo yasiyoridhisha ya timu zao kwenye fainali za AFCON mwaka huu.

ULE msemo unaopendwa kutumiwa na Waingereza kwamba ‘makocha huajiriwa ili watimuliwe’, umeendelea kudhihirika kupitia Fainali za Afcon 2019, baada ya makocha kachaa akiwamo wa Tanzania, Emmanuel Amunike kuliwa vichwa fasta.

Jana Jumatatu Shirikisho la Soka nchini (TFF) lilitangaza kufikia makubaliano ya kuvunja mkataba na Kocha Amunike ikiwa ni wiki moja baada ya timu hiyo kutupwa nje ya Afcon 2019 inayoendelea huko Misri.

Katika fainali hizo, Stars ilishika mkia baada ya kumaliza ikiwa haina pointi, ikipoteza mechi zote tatu za kundi C dhidi ya Senegal, Kenya na Algeria, ikifunga mabao mawili na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara nane (8)

Amunike (48) atakumbukwa kwa kuiongoza Taifa Stars kufuzu fainali hizo baada ya kusubiri kwa miaka 39, tangu ilipofanya hivyo kwa mara ya mwisho mwaka 1980.

Uamuzi wa TFF kuvunja mkataba na Amunike ni mwendelezo wa nuksi ambayo makocha wameendelea kukutana nayo baada ya baadhi ya timu zao kutofanya vizuri kwenye mashindano hayo ambayo sasa yanaingia hatua ya robo fainali.

Mwanaspoti linakuletea orodha ya makocha ambao tayari wameshatimuliwa na wale waliokalia kuti kavu kutokana na matokeo yasiyoridhisha ya timu zao kwenye fainali za AFCON mwaka huu.

JAVIER AGUIRRE - MISRI

Moja ya timu ambazo zilikuwa zinapewa nafasi kubwa ya kutamba na kutwaa taji kwenye fainali za AFCON mwaka huu ni waandaji, Misri kutokana na rekodi nzuri waliyonayo pindi wanapokuwa wenyeji lakini pia hata ubora wa kikosi chake.

Walianza vyema mashindano kwa kuongoza kundi A lililokuwa pia na timu za Uganda, DR Congo na Zimbabwe baada ya kushinda mechi zote tatu, wakifunga mabao matano na kutoruhusu nyavu zao zitikiswe hata mara moja.

Hata hivyo, walijikuta wakiondolewa kwenye hatua ya 16 Bora baada ya kuchapwa bao 1-0 dhidi ya Afrika Kusini ambayo hakuna aliyekuwa akiipa nafasi na sio kuchapwa tu bali hata kwenye mchezo wenyewe walionekana kupotezwa vibaya.

Kichapo hicho cha bao 1-0, kilisababisha Rais wa Chama cha Soka Misri (EFA), Hany Abou-Rida kutangaza kujiuzulu huku akimtimua kocha mkuu, Javier Aguirre, raia wa Mexico na kuvunja benchi lote la ufundi ambalo ndani yake pia lilikuwa na beki wa zamani wa Real Madrid ya Hispania, Michel Salgado.

Lakini pia pamoja na Abou-Rida kujiuzulu, pia wajumbe wawili wa kamati ya utendaji ya EFA, Hazem Emam na Ahmed Megahed nao walichukua uamuzi kama huo.

Sebastien Desabre - Uganda

Uganda ni timu ambayo ilionyesha kiwango bora kwenye fainali za AFCON mwaka huu kwa kucheza soka safi na la ushindani dhidi ya timu zenye wachezaji wa daraja la juu na ilifanikiwa kutinga hatua ya 16-Bora ambako walitolewa dhidi ya Senegal kwa kipigo cha bao 1-0.

Hata hivyo, licha ya wengi kuamini kuwa Uganda wanastahili sifa kwa kile walichokifanya kwenye AFCON, kocha wake mkuu, Sebastien Desabre hakubaki salama kwani mkataba wake na Shirikisho la Soka Uganda (FUFA) ulivunjwa kwa makubaliano binafsi baada ya kuinoa timu hiyo kwa miaka miwili.

Hata hivyo, kocha huyo amepata dili nono la kujiunga na klabu tajiri nchini Misri ya Pyramids ambayo atainoa kwa ajili ya msimu ujao.

Herve Renard - Morocco

Morocco ilikuwa inapewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa mashindano hayo baada ya kutamba kwenye hatua ya makundi, ikishinda mechi zote tatu ilizocheza dhidi ya Namibia, Ivory Coast na Afrika Kusini, tena bila ya kuruhusu goli hata moja.

Hata hivyo, ilikwama mbele ya Benin katika hatua ya 16-Bora baada ya kuchapwa kwa mikwaju ya penalti 4-1 kufuatia timu hizo kwenda sare ya bao 1-1 katika dakika 120 za mchezo.

Inadaiwa kuwa yuko mbioni kutimuliwa na uongozi wa Chama cha soka Morocco, ingawa bado taarifa hizo hazijawa rasmi.

Mbali na hao, makocha wengine ambao wamekalia kiti cha moto ni Sebastien Migne (Kenya), Clarence Seedorf (Cameroon), Ninguyeko Olivier (Burundi), Sunday Chidzambwa (Zimbabwe) na Florent Ibenge (DR Congo).