Ozil kufyekwa tena Arsenal

Muktasari:

Ozil alikuwa mmoja wa wachezaji waliogoma kukatwa mshahara wake ili kupunguza makali ya janga la corona ndani ya Arsenal

London, England. KAMA ni gundu basi hili la Mesut Ozil ni balaa aisee. Licha ya kulipwa mshahara mkubwa lakini Ozil amekuwa na maisha magumu kwenye kikosi cha Arsenal.

Tangu kuondoka kwa Arsene Wenger aliyemnunua kwa dau la rekodi ya klabu wakati huo kutoka Real Madrid, Ozil amekuwa hana nafasi kwenye kikosi hicho akisugua benchi na sasa balaa zaidi linamuangukia.

Kwanza, alianza kwa kuwekwa pembeni kwenye orodha ya wachezaji watakaoshiriki Europa League, ambapo hakuweza kupenya kwenye kikosi cha wachezaji 25.

Hata hivyo, wakati akiugulia maumivu hayo chini kwa chini, mapema leo Jumanne Oktoba 20, 2020 ikabainika kwamba, Ozil anaweza asiwemo kwenye kikosi cha wachezaji 25 watakaoshiriki Ligi Kuu England.

Kwa mujibu wa ESPN, imebainika kuwa jina la Ozil,32, halimo kwenye orodha ya wachezaji wa Arsenal jambo ambalo limezidi sintofahamu kuhusu mustakabali wake pale Emirates.

Kanuni za Ligi Kuu England zinazitaka klabu kuwasilisha majina 25 ya wachezaji wake, ambapo kati yao 17 ni lazima wawe wazawa na hapo ndipo Ozil anapoingia kwenye majanga.

Hata hivyo, kuna mazungumzo yanaendelea baina ya mabosi wa Arsenal na wawakilishi wa Ozil kuangalia namna bora ya kuvunja mkataba, ambapo hilo linaweza kutokea kwenye dirisha dogo la Januari.

Kutokana na hilo, Kocha Mikel Arteta amemuondoa kabisa mshindi huyo wa Kombe la Dunia mwaka 2014 kwenye mipango yake huku baadhi ya wachezaji na Wenger mwenyewe wakimpigia chapuo apewe nafasi.

Ozil, ambaye alitua Arsenal akiwa kwenye ubora wake, hajacheza tangu mwezi Machi, mwaka jana wakati Arsenal ikishinda bao 1-0 dhidi ya West Ham United.

Mbali na Ozil anayelipwa mshahara wa pauni 350,000 kwa wiki, Arsenal pia imeliondoa jina la beki wake wa kati Sokratis, ambaye hayumo kwenye kikosi cha Europa wala Ligi Kuu England.