Dube apewa mechi 6 Azam

Muktasari:

HAKUNA utata kwamba kwa muda huu mabosi wa Azam wana furaha kubwa juu ya usajili wa mshambuliaji wao mpya, Prince Dube kutokana na kuanza kwake vizuri Ligi msimu huu akiwa amefunga magoli mawili katika mechi mbili za Ligi Kuu.

Hilo pia hata kwa upande wa kocha mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba na yeye ameonyesha kufurahishwa na kiwango cha mchezaji huyo kwa kuanza vizuri Ligi.

“Prince ni mchezaji ambaye Azam tulikuwa tunamuhitaji, lakini ni mapema sana kwa sasa tusubiri mpaka mechi sita zipite ndio nitamzungumzia zaidi,” alisema kocha huyo raia wa Romania.

Akizungumzia baadhi ya nyota wake Ally Niyonzima na Shaban Chilunda kutoonekana kabisa hata benchi katika mechi mbili za mwanzo, Cioaba alisema wachezaji hao walikuwa na majeruhi.

“Kila mchezaji katika kikosi hiki atapata nafasi ya kucheza, hao walikuwa majeruhi lakini watapata nafasi ya kucheza wakiwa fiti wote kwa pamoja” alisema.

Hata hivyo. kwa upande wa Niyonzima yeye tayari alishaanza mazoezi na wenzake na anatarajiwa kujumuishwa katika kikosi kitakachoenda Nyanda za Juu Kusini.

Akizungumzia upande wa timu ngumu ambayo amekutana nayo katika mechi mbili za mwanzo, Cioaba aliitaja Polisi Tanzania kuwa timu yenye nguvu muda wote.