Mwamnyeto? Yanga ongezeni pesa kwanza

Muktasari:

COASTAL Union wameona beki wao wa zamani, Bakari Mwamnyeto alivyonoga kwenye ukuta wa Yanga wakaingia tamaa kutaka jamaa wawaongeze mkwanja.

COASTAL Union wameona beki wao wa zamani, Bakari Mwamnyeto alivyonoga kwenye ukuta wa Yanga wakaingia tamaa kutaka jamaa wawaongeze mkwanja.

Mwenyekiti wa Coastal Union, Steven Mnguto ameiambia Mwanaspoti kuwa; “Tunajua Yanga hawawezi kuwa waungwana. Ingekuwa inawezekana wangetuongezea fedha, Bakari ni beki bora sana na sasa watu wameona wenyewe kile tulichokuwa tunasema.”

Mnguto ambaye ni Mwenyekiti pia wa Bodi ya Ligi (TPBL), aliongeza kuwa Yanga watafaidi zaidi kutokana na umri wa beki huyo na kwamba pia atakapoanza kucheza mechi za kimataifa ataimarika zaidi.

“Watu waliona kama tunatania tukisema huyu ni beki ghali, tuliona kipaji chake na tunamfuatilia kila hatua kule Yanga na tunaongea naye pia kumpa nguvu ya kupambana zaidi.

“Tumeona alivyo na ubora wa kukabiliana na mipira ya juu sio rahisi ipigwe krosi halafu upite kwake kabla hajaugusa na kutibua, angalia pia anavyokuwa na utulivu miguuni kwa mipira ya chini.

“Tumewapatia beki mzuri lakini pia anaocheza nao pale Yanga ni wazuri na niseme sasa Yanga inacheza mashindano ya ndani wakija mashindano ya kimataifa atakuwa ameshaiva zaidi, kule atapata nafasi ya kujiongezea ubora zaidi,” aliongeza.

Mwamnyeto amecheza mechi zote za Yanga tangu aliposajiliwa akionekana kujihakikishia namba katika beki ya kati akishirikiana na Mghana Lamine Moro.