Mambo yameiva huko Thiago kutua Liverpool

Muktasari:

Thiago yupo kwenye hatua za mwisho kuondoka Bayern baada ya kukaa katika viunga hivyo kwa miaka saba na kuiwezesha kuchukua mataji kadhaa ya Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Ulaya ambalo ilichukua msimu uliopita.

LIVERPOO, ENGLAND

SIKIA hii, baada ya fununu za muda mrefu sasa mambo ni hadharani, Liverpool inaripotiwa kufikia makubaliano na Bayern Munich ili kufanikisha usajili wa Thiago Alcantara katika dirisha hili la usajili kwa ada ya usajili ya Pauni 26 miloni.

Thiago yupo kwenye hatua za mwisho kuondoka Bayern baada ya kukaa katika viunga hivyo kwa miaka saba na kuiwezesha kuchukua mataji kadhaa ya Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Ulaya ambalo ilichukua msimu uliopita.

Jurgen Klopp amewahi kunukuliwa mara kadhaa juu ya kauli zake za kutamani kuipata huduma ya mwamba huyo mwenye umri wa miaka 29, katika kikosi chake kwa msimu ujao.

Mazungumzo kati ya klabu hizo mbili yanatajwa kumalizika usiku wa juzi na Bayern imeripotiwa tayari kumuuza kwa kile kinachoeleza Thiago ameleta ugumu kwenye kusaini mkataba mpya ambao ilimuwekea mezani mwezi Mei, hivyo inahofia kumpoteza bure katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi au kumuuza kwa bei ya chini zaidi katika dirisha dogo la mwezi Januari.

Hiyo imeifanya Liverpool kuwa na jeuri na kusema haitatoa pesa ndefu ili kumsajili Thiago, ambaye atakuwa anafikisha umri wa miaka 30, mwezi April mwakani.

Vyanzo vya karibu kutoka kwa mchezaji huyo vinadai anafikria zaidi kuondoka Ujerumani lakini kikwazo imekuwa ni familia yake ambayo imemuambia inafuraha kuendelea kuwa katika nchi.

Katika moja ya mahojiano aliyofanya Thiago alikaririwa akisema Bayern ni nyumbani kwake na ana furaha zaidi kuendela kucheza hapo licha ya kuwepo kwa tetesi zinazomhuisha na kutaka kuondoka.

Lakini asilimia za staa huyo kuwepo Bayern kwa msimu ujao zinapungua zaidi ni kutokana na mipango ambayo imeanza kupangwa na kocha, Hansi Flick ambaye ameanza kujiandaa na maisha bila ya Thiago kwa kuanza kuwachezesha Joshua Kimmich na Leon Goretzka ambao wameanza kucheza pamoja katika eneo la kiungo.

Flick aliwahi kusema maneno ambayo yaliashiria ufinyu wa kusalia kwa Thiago.