MAMBO YA FEDHA: WAGENI WANAVYOCHANGIA KUKUA KWA UCHUMI KUPITIA SOKA

JUMLA ya wafanyakazi 81 wa kigeni kutoka nchi mbalimbali wapo nchini kwa ajili ya kucheza soka katika ligi mbalimbali zilizo chini ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) pamoja na mabenchi ya ufundi.

Hizo ni Ligi Kuu Bara, Daraja la Kwanza (FDL), Daraja la Pili (SDL) na Ligi Kuu ya Wanawake.

Katika ligi hizo nyota wote wa kigeni na makocha wao wanalazimika kulipa gharama mbalimbali ili wafanye kazi zao.

Wafanyakazi hao hulazimika kulipa gharama ya vibali vya kazi ambapo kila mmoja hulipa Dola 1,000 za Marekani ambazo hulipwa Wizara ya Kazi na Ajira na leseni ambayo kila mchezaji hulipa Sh4 milioni.

Vibali vya makazi hutolewa na Idara ya Uhamiaji kila mmoja ni Dola 550 kwa wale wanaotoka nchi za Afrika Mashariki na Kati, huku wanaotoka nje ya nchi hizo hulipa Dola 2,050 kila mmoja - wote ni kwa miaka miwili.

Hata hivyo, Chama cha Makocha Tanzania (Tafca) kimewasaheme makocha wa kigeni kulipa ada ambapo wazawa hulipa Sh24,000 kwa mwaka huku kila mwezi ni Sh2,000.

Katibu mkuu wa Tafca, Michael Mbundala anasema: “Tuliangalia kwa mapana zaidi upande wa makocha wa kigeni, huwa wanalipa gharama nyingi mpaka kuanza kazi, hivyo huku tumewasamehe ingawa tunawahesabu kama wanachama wetu.”

Mamilioni Uhamiaji

Zaidi ya Sh224 milioni zinakusanywa na Idara ya Uhamiaji kutokana na malipo ya vibali vya makazi kwa wafanyakazi wa klabu mbalimbali za soka nchini.

Wageni waliotoka nchi za Afrika Mashariki na Kati wamelipiwa vibali vya makazi vyenye thamani ya zaidi ya Sh49 milioni ambapo kila mmoja ni Dola 550 wakati zaidi ya Sh175 milioni ni kutoka wa wageni ambao ni wa nje ya nchi hizo.

Simba, Yanga, Azam ni noma Uhamiaji

Simba na Yanga ndizo zinaonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa kwa watumishi wao kutoka Afrika Mashariki na Kati ukilinganisha na timu nyingine kwa upande Mashariki na Kati kwa vibali vya makazi ambavyo hutolewa na Uhamiaji.

Lakini, Simba na Azam ndizo zinaonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa upande wa vibali vya makazi kwa wafanyakazi wanaotoka nje ya nchi za Afrika Mashariki na Kati kutokana na idadi ya wafanyakazi walionao.

Simba na Yanga zina idadi sawa ya wachezaji wa kigeni kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati ambapo kila moja ina wafanyakazi sita na kila mmoja hulipiwa Dola 550 kwa miaka miwili ambapo kila timu hulipa jumla ya Sh7,543,00 wakati Azam ina wafanyakazi watatu kutoka nchi hizo ambapo hulipa Sh3,771,900.

Kwa upande wa wafanyakazi wa kigeni kutoka nchi nyingine Simba na Azam FC zinalipa zaidi Uhamiaji ambapo timu zote mbili zina jumla ya wafanyakazi 20 huku kila timu ikiwa na wafanyakazi 10. Malipo ya vibali vya makazi ni Dola 2050 kwa kila mfanyakazi ambazo hulipwa kwa miaka miwili, hivyo kila timu imelazimika kulipa Sh46,863,000 ambazo jumla yake kwa timu zote mbili ni zaidi ya Sh94 milioni wakati Yanga ina wachezaji wanane ambapo hulipa zaidi ya Sh37 milioni.

Biashara United yenye wafanyakazi watano wa kigeni kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati inashika kasi katika ulipaji wa vibali vya makazi kwa wafanyakazi wake ambapo hulipa Sh6,286,500 kwa wachezaji hao huku ikilipa zaidi ya Sh9 milioni kwa wale wanaotoka nje ya nchi hizo.

Namungo FC ambayo huu ni msimu wake wa pili kwenye Ligi Kuu ina wafanyakazi wanane wa kigeni ambapo wanne hulipiwa zaidi ya Sh5 milioni kwa wanaotoka Afrika Mashariki na Kati huku wanne hulipiwa vibali vya makazi zaidi ya Sh15 milioni.

KMC, Sisterz FC nazo zimo

Watoto wa Kinondoni, KMC, ina wacheza watatu wa kigeni kutoka Afrika Mashariki na Kati ambapo huwalipia zaidi ya Sh3 milioni kwa miaka miwili, huku timu ya wanawake ya Sisterz FC ikiwa na wachezaji watano kutoka nchi hizo ambapo huwalipia zaidi ya Sh6 milioni kwa ajili ya vibali vya kazi.

Timu zingine zinazochangia uchumi wa taifa kupitia vibali vya makazi ni Kagera Sugar ambayo ina wachezaji wawili wa kigeni wanaolipa zaidi ya Sh2 milioni huku Mtibwa Sugar ikiwa na mmoja inayemlipia zaidi ya Sh1 milioni, timu zote mbili zina wachezaji kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Gwambina FC inayoshiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza imeajiri wawili kutoka nje ya nchi za Afrika Mashariki ambapo huwalipia vibali vya makazi zaidi ya Sh9 milioni huku Dodoma Jiji ina mmoja inayemlipia zaidi ya Sh4 milioni sawa na Kitayosa FC ambayo pia ina mchezaji mmoja.

Singida United imetia fola FDL kwa kuwa na nyota wengi wa kigeni ambapo inalipa zaidi ya Sh18 milioni kwa wanne wanaotoka nje ya nchi za Afrika Mashariki na Kati, huku mmoja ndiye hulipiwa zaidi ya Sh1 milioni. Timu ya wanawake ya TSC ina wachezaji wawili wa kigeni ambao wote wanatoka nchi za Afrika Mashariki na Kati, hivyo hulipa zaidi ya Sh2 milioni.

Wasikie uhamiaji

Akizungumza na Mwanaspoti, msemaji mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Paul Mselle anasema: “Ni jukumu la kila mmoja kulipia kibali cha makazi, hivi vibali huombwa kwa njia ya mtandao.”

“Ili apate kibali cha makazi ni lazima awe amepata kibali cha kazi, hivyo tuliwakumbusha TFF kuwaambia wanachama wao kuhakikisha kila mfanyakazi wa kigeni anafuata taratibu za kuwa na kibali kitakachomruhusu kuishi nchini vinginevyo inakuwa ni kinyume na sheria za nchi.

“Hivyo naamini kila klabu ama kila mfanyakazi mpaka sasa ametekeleza hilo, kwanza amepata kibali cha kazi, pia amelipia kibali cha makazi ambapo kibali cha makazi hulipwa kwa dola. Kwa wale wanaotoka nchi za Afrika Mashariki na Kati ni Dola 550 na wote wa nje ya nchi hizo wakiwemo wale wa nchi za SACD gharama yao ni moja ambayo ni Dola 2,050 kwa miaka miwili.”

Wizara ya Kazi na Ajira

Ligi zote ambazo zipo chini ya TFF ambazo ni Ligi Kuu Bara, FDL, SDL na Ligi Kuu ya Wanawake zina jumla ya wafanyakazi 81 wa kigeni ambao ni wachezaji na wataalamu mbalimbali wa mabenchi ya ufundi. Viongozi wa klabu husika ambazo zimeajiri wachezaji na makocha wa kigeni wanalazimika kuwalipia vibali vya kazi watumishi wao kwenye Wizara ya Kazi na Ajira ambapo kila mmoja hulipiwa Dola 1000, hivyo jumla yake kwa wafanyakazi hao viongozi wa klabu mbalimbali huilipa serikali zaidi ya Sh187 milioni. Simba, Yanga na Azam FC ndizo zinazoongoza kupandisha uchumi wa nchi kupitia ada za vibali vya kazi kwa wafanyakazi wao kutokana na kuajiri idadi kubwa ya wafanyakazi wa kigeni.

Shirikisho la soka

Idadi ya wafanyakazi wa kigeni kwenye sekta ya soka kwa ligi zote ni 81, lakini kati ya hao 11 ni wataalamu kwenye mabenchi la ufundi, hivyo wafanyakazi 70 ni wachezaji. Kwa mujibu wa kanuni za TFF ni lazima klabu walipie wachezaji wake ada ya leseni ambayo ni Sh4 milioni kwa kila mmoja, hivyo shirikisho hilo linakadiriwa kukusanya Sh280 milioni kwani makocha na wataalamu wengine hawalipiwi leseni hizo.

Viongozi wafunguka

Mkurugenzi wa Singida United ambayo imeshuka daraja, Yusuph Mwandami anasema: “Ni gharama kubwa tunalazimika kulipia wachezaji wetu, tuna wachezaji kama watano wa kigeni ambao kwa vyovyote vile lazima tuwalipie vibali vya kazi na makazi na mambo mengine.

“Tumeshuka daraja na tuna wakati mgumu kiuchumi ambapo hatudhani kama tunaweza kumudu yote hayo huku matarajio yetu ni kupunguza matumizi, kinachotugharimu nchi nyingi hawajafungua mipaka baada ya kuwepo na janga la virusi vya corona.

“Vinginevyo hata hawa waliopo tungekuwa tumewarudisha kwao, lakini hivi inakuwa vigumu ila tutaona namna ya kufanya, kwani tunahitaji wachezaji wengi wazawa kwa sasa.”

Simba

Wachezaji kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati ndani ya Simba wako sita, upande wa wanaume ni Meddie Kagere, Joash Onyango na Francis Kahata ilhali kwa wanawake (Simba Queens) ni Bertha Odhiambo (Kenya), Asha Djafari na Joelle Bukuru (Burundi).

Kutoka nje ya Afrika Mashariki ikiwemo zile nchi za SADC ni Pascal Wawa, Bernard Morrison, Larry Bwalya, Chris Mugalu, Luis Miquissone, Clatous Chama na Gerson Fraga.

Watalaamu wa benchi la ufundi ni kocha mkuu Sven Vandenbroek, kocha wa viungo Adel Zrane na mtaalamu wa tiba za viungo Paulo Gomez.

Yanga

Wachezaji wa timu ya wanaume kutoka Afrika Mashariki na Kati katika kikosi cha Yanga ni Farouk Shikalo (Kenya), Haruna Niyonzima (Rwanda) na upande wa timu ya wanawake ya Yanga Princess ni Aniella Uwiwana, Janeth Moraa na Wincate Kaari wote kutoka Kenya na kocha wa makipa kutoka Burundi, Vladmir Niyonkuru.

Nchi nyingine ni Michael Sarpong (Ghana), Songne Yacouba (Burkina Faso), Tonombe Mukoko, Tuisila Kisinda (Congo), Lamine Moro (Ghana), Carlos Sténio Fernandes ‘Carlinhos’ (Angola) na benchi la ufundi lina kocha mkuu Mserbia, Zlatko Krmpotic.

Azam FC

Azam FC kutoka Afrika Mashariki na Kati ni Nico Wadada (Uganda), Ally Niyonzima (Rwanda) na kocha msaidizi kutoka Burundi, Vivier Bahati.

Nchi nyingine ni Daniel Amoah (Ghana), Bruce Kangwa (Zimbabwe), Yakubu Mohamed (Ghana), Alain Thierry Akono (Cameroon), Prince Dube (Zimbabwe), Richard Djodi (Ivory Coast), Obrey Chirwa (Zambia), Never Tigere (Zimbabwe).

Benchi la ufundi ni kocha Aristica Cioaba na Costel Birsan kutoka Romania.

Namungo FC

Namungo FC ina wafanyakazi wanane - kocha wao Thiery Hitimana (Rwanda) na wachezaji ni Bigirimana Blaise, Jonathan Nahimana, Styve Nzigamasabo (Burundi) huku nchi nyingine ni Joseph Quansah, Stephen Duah na Stephen Kwame Sey (wote kutoka Ghana) na Balora Nouridine wa Burkina Faso.

Bishara United

Biashara United ina wafanyakazi saba - kocha mkuu Francis Baraza (Kenya), wachezaji ni Ambrose Awio, James Ssetuba na Joseph Zziwa (Uganda) na Timoth Omwenga (Kenya) ilhali nje ya Afrika Mashariki na Kati ni Abdulwaheed Yusuf (Nigeria), na Christian Zagah (Ghana).

KMC

KMC inayomilikiwa na Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam ikiwa ni msimu wake wa tatu kwenye Ligi Kuu Bara ina wachezaji watatu wa kigeni ambao ni Yussuf Ndikumana na Emmanuel Mvuyekuru (Burundi) na Jean Mugiraneza (Rwanda).

Kagera Sugar

Kagera Sugar yenye maskani yake mkoani Kagera na iko chini ya kampuni - nayo imesajili nyota wawili wa kigeni ambao ni Jackson Harodi kutoka Uganda na Mosi Hadji wa Burundi.

Gwambina FC

Ni timu iliyopanda daraja msimu huu na imesajili mchezaji mmoja wa kigeni kutoka Zimbabwe ambaye ni Stali Nyambe na mkurugenzi wa ufundi kutoka DR Congo, Mwinyi Zahera.

Mtibwa Sugar

Mtibwa Sugar ambayo ilikuwa haisajili wachezaji wa kigeni, lakini tangu msimu uliopita walimsajili mchezaji kutoka Uganda, Boban Bogere.

Mbeya City

Miaka kama miwili iliyopita, Mbeya City ilikuwa miongoni mwa timu ambazo zinasajili nyota zaidi ya wawili kutoka nje ya nchi, lakini tangu msimu uliopita wanaye mshambuliaji mmoja pekee kutoka Nigeria, Abasirim Chidiebere.

Dodoma Jiji

Ni timu ngeni kwenye Ligi Kuu iliyopanda msimu huu makazi yake yakiwa jijini Dodoma na inamilikiwa na Manispaa ya Dodoma ikiwa imesajili mchezaji mmoja wa kigeni kutoka Nigeria, Michael Chinedu.

Daraja la Kwanza (FDL)

Kwenye Ligi Daraja la Kwanza (FDL), Singida United imesajili wachezaji wa kigeni watano ambao ni Owen Chaima (Malawi), Chikondi Daka (Zambia), David Nartey (Ghana), Herman Frimpong (Ghana) na Seiri Arigumaho

Uganda

Kitayose FC yenyewe ina mchezaji mmoja wa kigeni kutoka Ghana, Stephen Opoku.

6- Sisterz FC

Wafanyakazi wa kigeni wa timu hiyo kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati ni Clementine Mukamana, Pauline Jeanne (wote kutoka Rwanda), Nasra Nahimana, Esta Nzeyimana, Rachele Bukuru na Neema Nshimirimana wanaotoka Burundi.

TSC Queens

TSC inashiriki Ligi Kuu ya Wanawake ina wachezaji wawili wa kigeni ambao ni Rachelle Bukuru na Neema Nshirimana.