Kiduku amdai Mbabe pesa, afunguka kutovikwa mkanda

Saturday August 29 2020

 

By Imani Makongoro

Baada ya kipigo, Twaha Kiduku amemtaka, Dullah Mbabe kutimiza ahadi yake aliyosema kama atampiga atampa Sh200,000 huku akianika sababu ya kutovikwa mkanda wa ubingwa.

Kiduku amemchapa Mbabe kwa pointi za majaji wote watatu ambao walimpa pointi 97-93, 99-91 na 97-93 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo Jumamosi.

Kiduku aliongoza raundi zote 10 za pambano hilo la kuwania ubingwa wa Taifa katika uzani wa Super Middle.

Hata hivyo bondia huyo pamoja na Ibrahim Class ambaye alishinda ubingwa wa Taifa katika uzani wa Super Feather hawakupewa mikanda baada ya pambano hilo.

"Shida yangu haikuwa mkanda, nilitaka nimpige tu ili nimfunge mdomo, japo mimi ndiye nilikuwa nautetea ubingwa huo," anasema Kiduku.

Anasema hata hivyo hakuvalishwa mkanda huo kwa kuwa haukuwepo uwanjani hapo, kauli sawa na iliyotolewa na Ibrahim Class.

Advertisement

Kaimu rais wa TPBRC, Agapeter Mnazareth amesema mikanda yao ipo na watapewa.

"Huenda hawakuvalishwa kutokana na mazingira, lakini ipo watapewa, licha ya kutopewa uwanjani, lakini katika rekodi ndiyo mabingwa wetu."

Katika hatua nyingine, Twaha Kiduku amemtaka Mbabe kutimiza ahadi aliyoitoa kuwa kama atapigwa na Kiduku basi atatoa Sh 200,000 kumpa.

"Atimize ahadi yake sasa, "Nilimwambia nitampiga kama 'begi' akawa anachoonga na kujitapa kuweka pesa mezani kama nikimpiga, sasa ziko wapi? atoe sasa hizo pesa," alisema Kiduku.

Mbabe alitoa kauli ya kumpa pesa hiyo Kiduku wiki kadhaa kabla ya pambano walipokutana kwenye mkutano na waandishi wa habari, Serena hoteli jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo Mbabe hakutaka  kuzungumzia ahadi hiyo wala chanzo cha kipigo hicho ambacho kilipokelewa kwa mikono miwili na pande zote mbili.

Tangu raundi ya kwanza hadi ya mwisho, Twaha alioneka mtulivu muda wote, akirusha ngumi za malengo ambazo nyingi zilimlenga Mbabe usoni, ingawa alijibu mapigo lakini ngumi zake nyingi hazikuwa za malengo na nyingine zikiishia hewani kutokana na umahiri aliouonyesha Twaha katika kukwepa.

Raundi ya sita na ya nane, Mbabe alikubali mashambulizi mfululizo huku mashabiki wa Twaha wakisimama na kushangilia wakitarajia matokeo ya KO, lakini ilikuwa tofauti baada ya bondia huyo kuokolewa na kengere.

Mara kwa mara Mbabe alionekana kutaka huruma ya refarii huku kuna raundi alijikuta akionyesha ishara kwa mashabiki katikati ya mchezo tofauti na Kiduku ambaye alitulia na kucheza ngumi mwanzo mwisho bila kuzungumza na refarii wala mashabiki zaidi ya wasaidizi wake wa ulingoni (seconds) walioongozwa na kocha wake, Power Ilanda.

Bondia aliyekuwa akimsapoti Mbabe, Japhet Kaseba baada ya pambano hilo alikiri kambi yake kuzidiwa.

"Ndio mchezo ulivyo, Twaha ameshinda kihalali, Mbabe inaonekana alizidiwa, lakini ajipange upya,"

Advertisement