Gumzo duniani, Messi, Ronaldo kucheza pamoja Juventus

Tuesday July 7 2020

 

SOKA halina msamiati unaosema “haiwezekani”. Kila kitu kinawezekana. Manchester City wamewachapa mabingwa wa England, Liverpool 4-0. Siku chache baadaye wanachapwa 1-0 na Southampton. ‘Haiwezekani’ haijawahi kuwapo kwenye mchezo wa soka. Na sasa kinachosemana ni kwamba mpango uliopo ni kuwafanya masupastaa wawili, Lionel Messi na Cristiano Ronaldo kucheza pamoja, kwenye kikosi kimoja.

Awali ilidaiwa kwamba David Beckham anaweza kuwafanya mastaa hao kucheza pamoja kwenye timu yake ya Inter Miami huko Marekani, watakapoona soka la Ulaya limewachosha, lakini kinachoelezwa jambo hilo linaweza kutokea mwakani tu hapo – Messi akipelekwa Turin kukipiga na Ronaldo kwenye chama la Juventus.

Kinachoripotiwa ni kwamba Messi na Ronaldo wanaweza kukipiga pamoja kwenye kikosi cha Juventus kama tu mawakala watataka jambo hilo

litimie kabla ya wawili hao kustaafu soka. Supastaa wa Kiargentina, mshindi mara sita wa Ballon d’Or, Messi anajiandaa kuachana na Barcelona mwakani.

Kutokana na hilo, Messi na Ronaldo wanaweza kucheza pamoja kwenye kikosi cha Juventus msimu wa 2021/22.

Staa wa zamani wa Brazil na Barcelona, Rivaldo alisema kwamba mawakala wa soka wapo kwenye mchakato mahususi kabisa wa kumfanya Messi timu yake ijayo atakayokwenda kucheza iwe Juventus. Dhamira ya kufanya hivyo kuona Juventus ikiandika historia ya kuwa na wachezaji wawili mastaa wa dunia wakicheza pamoja kwenye kikosi chao.

Advertisement

Kinachoelezwa huko Hispania ni kwamba Messi, 33, atabaki tu Nou Camp kama swahiba wake Xavi Hernandez atarudishwa kwenye timu hiyo na kupewa mikoba ya ukocha.

Messi na Ronaldo wamechuana kuwania umwamba wa dunia kwa miaka kibao waliyokuwa pamoja kwenye soka la Hispania.

Walikuwa kwenye mchuano mkali kila wiki hadi hapo Ronaldo, 35, alipohama Real Madrid na kwenda kujiunga na Juventus kwa ada ya Pauni 99 milioni mwaka 2018.

Na sasa, uwezekano wa kuwaona wawili hao wakicheza kwenye kikosi kimoja na kusimama kwenye fowadi ni kitu kinachosubiriwa kwa hamu kitokee ndani ya miaka michache ijayo. Kama dili hilo litafanikiwa mwakani, Messi atakuwa na umri wa miaka 34 na Ronaldo atakuwa ametimiza umri wa miaka 36.

Kila kitu kinaonekana kwamba hakuna ugumu wa kushindikana baada ya kituo kimoja cha redio huko Hispania, Cadena SER kuripoti kwamba Messi atabaki tu Barcelona hadi mwisho wa mkataba wake wa sasa anaolipwa Pauni 500,000 kwa wiki.

Mkataba wake utafika tamati mwishoni mwa msimu ujao.

Rivaldo amedai kwamba mawakala wanatumika kuhakikisha Messi anakwenda kutua Turin msimu ujao.

Mkali huyo wa zamani wa Nou Camp, Rivaldo alisema: “Kutokana na haya mambo, naamini kuna baadhi ya mawakala wamekuwa na mpango wa kwenda kuwafanya Messi na Ronaldo wacheze Juventus.

“Hicho kitu kitakuwa kikubwa sana duniani. Kama ikitokea basi kutakuwa na mtikisiko duniani na bila ya shaka Juventus watakuwa amerudisha nguvu yao kubwa kwenye uwekezaji kupitia Muargentina huyo, ndani na nje ya uwanja.

“Itakuwa jambo la kuhistoria kuona wachezaji hao wawili wakicheza pamoja na nina uhakika wadhamini wengi wa Juventus watapenda hilo litokee, hivyo watasaidia kutoa pesa, hivyo kuna uwezekano huo.

“Kama lisemwalo kwamba anataka kuondoka, hivyo, bila ya shaka kila klabu inahitaji kumsajili, itatazama namna ya kupata saini yake.

“Itakuwa gumzo, wachezaji wawili bora duniani waliotamba kwa miaka 10 kucheza kwenye timu moja ni habari kubwa.

“Kama Messi amepanga kuondoka Barcelona, basi kuna kitu hakipo sawa, amechoshwa na matatizo yaliopo kwenye timu.”

Messi anahusishwa pia na mpango wa kwenda Manchester City kwenda kuungana na kocha wake wa zamani, Pep Guardiola. Hata hivyo, dili dili linaweza lisitimie kama tu, Man City itakwenda kwenye rufaa yao ya kupinga kufungiwa kwa misimu miwili kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kwa msimu huu, Messi amefunga mabao 22 kwenye La Liga, wakati Ronaldo ametikisa nyavu mara 25 kwenye Serie A.

Advertisement