EXTRA SPESHO: Jide miaka 20 kwenye Bongofleva saluti kwako

Sunday June 07 2020
Jide pic

Lady Jaydee, Jide, Komando, Binti Machozi au Anaconda, muite utakavyo. Mimi namwita Legend.

Wakati tukisherehekea miaka 20 ya Judith Wambura Mbibo, nimejikuta nikikumbuka nilivyomfahamu na kisha kufahamiana na mwanadada huyu mchapakazi.

Mwishoni mwa mwaka 1999 wakati Joseph Mbilinyi a.k.a Sugu akiandaa albam yake ya tano ya ‘Millenia’ iliyotoka mwaka 2000, nilikuwa nikipiga stori mara kwa mara na rapa huyu gwiji Tanzania, ambaye kwa miaka 10 sasa ni Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini.

Katika wa kutangaza ujio wa albam yake ya ‘Millenia’, Sugu aliachia wimbo wa ‘Mambo ya Fedha’. Ilikuwa ni bonge moja ya ngoma, ngoma iliyostahili kutangaza ujio wa kishindo wa albamu mpya.

“Mambo ya Fedha, utafanya usiyoyaweza, utasema usiyoyaweza, mambo ya fedhaaa,” ilisikia sauti tamu na adimu sana katika kiitikio cha wimbo huo uliobamba vyema soko la Bongo Fleva.

Kila mmoja alikuwa akimfahamu Sugu kwa wakati huo. Hakuna aliyemshangaa kwa kuachia ngoma kali kama hiyo kwani alikuwa tayari ni staa mkubwa ambaye alishatamba na ngoma zake nyingi zilizokuwamo katika albam zake nne zilizotangulia za ‘Ni Mimi’ (1995), ‘Ndani ya Bongo’ (1996), ‘Niite Mr 2’ (1998) na ‘Nje ya Bongo’ (1999).

Advertisement

Mtu pekee aliyewastua watu, nikiwamo mimi, kuhitaji kumfahamu baada ya wimbo huo alikuwa ni aliyeimba kiitikio hicho.

Njia sahihi ya kumfahamu mwimbaji huyo, ilikuwa ni kupitia Sugu. Kwa kuwa wakati huo nilikuwa nikizungumza na kukutana na Suga mara kwa mara, katika stori zetu nikamuuliza ni nani muimbaji wa kiitikio hicho.

Sugu alinifahamisha kuhusu muimbaji huyo na ndio ikawa mara ya kwanza mimi kulisikia jina la Lady Jaydee. Lilikuwa ni jina jipya kwa sababu kwa wakati huo JD tuliyekuwa tukimfahamu katika anga la burudani Bongo alikuwa ni Dj JD, John Dilinga Matlou.

Baadaye nikafahamishwa kwamba Jide alikuwamo katika wimbo wa Mawingu wa kuomboleza kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliyefariki dunia Oktoba 14, 1999 ambao ulihusisha wasanii kibao akiwamo Fina Mango ambao waliimba ‘Tutaku-ku-mbukaaa Baba wa Taifa.”

Kwa kuwa wakati huo, Jaydee alikuwa akianza harakati zake za kimuziki, Ruge Mutahaba (sasa marehemu), aliniita katika ofisiza Clouds FM wakati huo zikiwa katika jengo la Kitega Uchumi lilipo Posta jirani na Chuo cha IFM na kunifahamisha mengi kuhusu Jaydee na nikakutana naye mwenyewe na nikafanya naye ‘interview’ ya kwanza mimi naye.

Baada ya kuandika makala ya Jide ambaye alikuwa hafahamiki ukiacha kuimba kiitikio cha wimbo ‘Mambo ya Fedha’ wakati huo nikiwa katika gazeti la LeteRAHA, sikuwahi kuona akiwa amehojiwa na kuandikwa makala magazetini hapo kabla. Alishaandikwa? Pengine.

Tangu hapo, Jaydee akaachia wimbo wake uliomtangaza sana wa ‘Machozi’ uliofuatana na video ile maarufu iliyomshirikisha mwanamitindo wa kiume wa wakati huo, Frank Mgoi aliyejikuta akifahamika zaidi mtaani kama Frank ‘Machozi’.

Chini ya Benchamark Production, ‘Machozi’ ilikuwa moja ya video bora zaidi kupata kutokea kwa wakati ule. Ukawa mwanzo wa kishindo sana wa Jaydee katika gemu na tangu hapo hajarudi nyuma. Baada ya kuachia albam za kutosha kuanzia ‘Machozi’ (2000), ‘Binti’ (2003), ‘Moto’ (2005), ‘Shukrani’ (2007), ‘Ya 5. The Best of Lady Jaydee’ (2012), ‘Nothing But The Truth’ (2013) hadi ‘Woman’ (2017), Jide ni mshindi zaidi ya tuzo 36 zikiwamo za ndani na za Afrika.

Juzi usiku katika mahojiano na TvE, Jide alisema mwanamuziki aliyechangia mafanikio yake ni gwiji wa Zimbabwe, Oliver Mtukudzi (sasa marehemu). Ndiye aliyemshauri apige muziki wa bendi. Aachane na mambo ya kutumia CD.

Alisema, mwaka 2001 akiwa ameachia albam yale ya ‘Machozi’, alikuwa bado ni underground. Alialikwa kwenye tuzo za muziki za Kora. Huko Afrika Kusini katika tuzo hizo alikuwapo pia Mtukudzi. Alisema alikuwa akimuangalia gwiji Mtukudzi kwa hofu.

Hata alipopata fursa ya kuongea na supastaa huyo wa wimbo ‘Neria’, alikuwa akitetemeka. Mtukudzi hakuwa mtu wa mchezo mchezo. Alikuwa ni supastaa wa kweli barani Afrika.

Hata hivyo, Jide alishangaa kuona gwiji huyo alikuwa mtu mzuri sana asiyejisikia. Alimpa ushauri mwingi ikiwamo kuacha kutumia CD na kuanza kupiga muziki wa live. Wasia ule muhimu ulibadili maisha ya kisanaa ya Jide. Tangu hapo yeye hutumbuiza na live band tu, Machozi Band.

Miaka saba baadaye akapata nafasi ya kufanya wimbo na legend huyu aliyefariki Januari mwaka jana.

Safu hii haitoshi kuandika kila kitu kuhusu Legend Jide. Ninachoweza kufanya hapa ni kukupigia saluti tu.

Advertisement