Yanga? Nimeanguka zangu Simba

Wednesday May 20 2020

 

By THOBIAS SEBASTIAN

YANGA walikuwa wakihusishwa na wachezaji mbalimbali ikiwemo winga matata wa Simba, Mkongomani Deo Kanda ambaye amefunguka kuwaacha kwenye mataa.

Mwanaspoti lilimtafuta Kanda na kumpata akiwa mazoezini kwenye fukwe za Bahari ya Hindi na kufunguka suala hilo pamoja na mambo mengine.

Kusaini Simba

Kanda ambaye aliingia Simba kwa mkataba wa mkopo wa miezi sita akitokea TP Mazembe, anasema ni kweli ameongeza mkataba mpya wa miaka miwili na Simba baada ya ule wa kwanza wa miezi sita kumalizika.

“Nimekubaliana na viongozi wangu wa Simba na tumekubaliana kuongeza mkataba wa miaka miwili na jambo hili limefanyika kimya kimya ila muda ukifika watalitangaza hilo,” anasema.

“Kwahiyo katika hili la mkataba wangu kumalizika hakuna tena lingine jipya kwani nishaongeza tayari mwingine wa miaka miwili na kuendekea kuitumikia timu hii,” anasema Kanda ambaye mchango wake ndani ya Simba msimu huu umekuwa kabambe.

Advertisement

KUITEMA YANGA

Kanda anasema wakati Yanga wakiwa kwenye harakati za kuanza kumfuatilia alikuwa akizungumza na Simba siku nyingi suala la kumwongeza mkataba.

Anasema ilikuwa ngumu kuachana na Simba halafu aende kujifunga kwenye timu nyingine ambayo ndio wapinzani wa Jadi wa timu hiyohiyo.

“Sikutaka kwenda mbali niliwaeleza tu kuwa sitaweza kwenda kokote zaidi ya kubaki hapa Simba ambao siku chache zijazo wameniongezea mkataba mwingine mpya.

“ Unajua katika kipindi cha usajili mchezaji kama ukiwa katika kiwango kizuri na mkataba wako umemalizika lazima uhusishwe na timu nyingine nyingi basi hilo ndio limenikuta nami,” anasema.

“Kwa maana hiyo mbali ya kuhusishwa na Yanga niliamua kuachana na hilo na kuongeza mkataba mpya Simba ambao naimani nitawapatia zaidi kile ambacho wanahitaji kutoka kwangu,” anasema Kanda.

MALENGO MAPYA

Anasema kubwa ambalo anatakiwa kulifanya hapa ni kuhakikisha Simba wanafanya vizuri katika mashindano ya kimataifa kwa maana hiyo ajitume na kupambana kadri ambavyo anaweza.

“Mashindano ya kimataifa Simba ndio malengo yake makubwa kufanya vizuri huko ndio maana nimebakishwa hapa kwa maana hiyo kulingana na uzoefu wangu ambao ninao nitahakikisha napambana kadri ambavyo naweza ili kuwa sehemu ya nilifanikisha hili.

“Malengo mengine ni kuwa katika sehemu ya mafanikio kwenye mashindano mengine kama kutwaa ubingwa wa ligi na mashindano mbalimbali ambayo tutakuwepo,” anasema Kanda.

KOMBE LA DUNIA

Desemba 2010, Kanda akiwa na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo walikuwa timu ya kwanza Afrika kuingia fainali za Klabu Bingwa ya Dunia, kwa kuicharaza mabingwa wa Copa Libertadores, Internacional ya Brazil, mabao 2-0. Hiyo ni kama kombe la Dunia la klabu.

TP Mazembe ambayo ni mabingwa wa Afrika, walicheza fainali mabingwa wa Ulaya, Inter Milan ya Italia na mabingwa hao wa Ulaya walishinda mabao 3-0.

Kanda alielezea kuwa ulikuwa mchezo mkubwa katika historia ya maisha yake pamoja na wachezaji wengine wote ingawa walishindwa kuchukua ubingwa na kushinda.

“Haikuwa kazi rahisi kwetu kushinda mchezo ule kutokana na ubora wa Milan, pamoja na aina ya wachezaji waliokuwepo katika kikosi chao lakini kubwa kilikuwa kitu kizuri kwetu kufika fainali na kuweka historia kubwa kwa upande wa Afrika,” anasema.

“Kipindi kile nilikuwa ndio nachipukia na walikuwepo wachezaji wakubwa katika kikosi chetu ndio maana wengine wameshastahafu ila mimi bado naendelea kucheza mpaka wakati huu,” anasema.

ISHU ZAKE

Mtandao wa wikipedia unaonesha Kanda amezaliwa Agosti 11, 1989 na mpaka sasa ana zaidi ya miaka 30.

Wachezaji wengi waliocheza fainali ya klabu bingwa dunia wameonekana kustaafu na kuendelea na shughuli nyingine huku Kanda akiwa bado anacheza soka.

Kanda anasema alianza kucheza soka, mwaka 2017-09 pale DC Motema Pembe akiwa bado ana umri mdogo ndio maana mpaka sasa bado anacheza soka.

“Nadhani naonekana nimecheza soka kwa muda mrefu kutokana nilianza kucheza tangu nikiwa na umri mdogo, lakini kwangu nimefanikiwa hili kwa sababu ya kujifunza.

“Muda mwingi huwa napumzika nafanya yale mambo ambayo nahitajika kufanya katika maadili yangu ya kazi na tofauti na hapo huwa sina mambo mengi zaidi ndio maana nimedumu katika soka mpaka sasa,” anasema Kanda.

KUONDOKA MAZEMBE

“Wakati mkataba wangu ukiwa unamalizika nilikutana na ofa ya Simba ambayo ilikuwa ngumu kuachana nao kwa wakati huo kutokana tu nacheza soka ili kupata kipato.

“Kuondoka Mazembe haikuwa rahisi kwani hata makocha na viongozi wa timu hiyo muda wote nimekuwa nikiwasiliana nao na walinipa baraka yakuja kucheza hapa Simba,” anasema Kanda.

“Mazembe ni timu kubwa yenye mafanikio mkubwa hapa Afrika na ambavyo nimeishi katika timu hiyo nadhani soka langu nitakwenda kuhitimishia hapo,” aliongezea.

“Sababu moja wapo ambayo ilinichangia kusaini au kukubali kucheza hapa Simba ni nafasi ya kucheza mashindano ya kimataifa kwa maana Ligi ya Mabingwa Afrika,” anasema.

“Unajua ukicheza mashindano hayo makubwa kwa ngazi ya klabu na ukafanikiwa kufanya vizuri inakuwa faida kubwa kwako kuonekana lakini hata timu kufanya vizuri pia,” anasema.

“Binafsi huwa sipendi kuona nipo katika huku hatuchezi mashindano ya kimataifa hili lilinigusa pia msimu uliopita timu yangu tulipoondolewa katika hatua ya awali kwenye mashindano haya,” anasema.

“Kiu ambayo tunayo wachezaji, makocha na viongozi wetu nadhani msimu ujao tutapiga hatua zaidi kwenye mashindano hayo makubwa Afrika kwa ngazi ya klabu,” anasema Kanda.

USHIKAJI NA MOLINGA, TSHISHIMBI

Kanda anasema mbali ya upinzani uliokuwepo kati yake na wachezaji wa Yanga, David Ndama Molinga na Papy Kabamba Tshishimbi wanapokutana uwanjani nje ya hapo ni marafiki mno.

“Molinga na Tshishimbi ni marafiki zangu mno na huwa tunatembeleana mno katika nyumba zetu ambazo tunaishi kila wakati tunapata nafasi ya kufanya hivyo,” anasema.

“Si umeona hata hapa mazoezini nilikuwa na Molinga basi hivyo ndio maisha yetu yalivyo ni watu wa karibu mno ukiondoa ushindani wa dakika 90, tunapokutana uwanjani,” anasema Kanda na kukiri kabla ya kusaini Simba timu kibao zilimpa ofa.

“Baada ya kufahamika mkataba wangu unamalizika nilipokea taarifa kutoka kwa wakala wangu kuwa kuna timu nyingi kutoka hapa Afrika na Ulaya ambazo si zile za madaraja ya juu,” anasema.

“Nilishauriana na wakala wangu na nikamueleza kuwa kwa ambavyo nimeishi Simba, nadhani tukubali kuongeza mkataba mwingine na kuachana na hizo ofa za timu nyingine na tukalifanya hilo,” anasema Kanda.

YEYE NA SVEN

Kanda anasema katika kipindi hiki ligi, imesimama amekuwa akikomaliwa na kocha wa timu hiyo Sven Vanderbroeck ambaye hataki mzaha hata kidogo.

Anasema ukifika muda wa kufanya mazoezi Sven, huwa anampigia simu (Video Call), kumpatia aina ya mazoezi ya kufanya.

“Wakati ananipatia aina ya mazoezi ambayo natakiwa kufanya muda huo huo ananiangalia na hata nikikosea huwa akaniambia nirudi kufanya tena,” anasema.

“Hata kama nikiwa nafanya mazoezi dakika 40, au zaidi muda wote nipo nae na ananifatilia hatua baada ya hatua kila siku na nifanye vile ambavyo anataka.

“Kiukweli Sven ananifuatilia muda wangu wote wa mazoezi, wakati huu nipo fiti kama ligi inaendelea vilevile,” anasema mchezaji huyo na kusisitiza kwamba kwa ubora wa Simba hadhani kama kuna wa kuwababaisha.

Advertisement