JICHO LA MWEWE: Maisha yalivyokwenda kasi kwa Ditram Nchimbi

KWA kuanzia tu. Kwa utani tu. Mabao yote mawili ya Taifa Stars dhidi ya Sudan pale ugenini yalifungwa na Wangoni.

Erasto Nyoni na Ditram Nchimbi. Ni miongoni mwa utani ambao ulikuwa unaendelea mitandaoni juzi.

Taifa Stars imefuzu kwenda Chan kwa mara ya pili. Jina la Nchimbi linaingia katika historia. Bao la kwanza lilitokana na yeye kukwatuliwa wakati akielekea katika lango la Sudan. Nyoni akapiga frii-kiki maridadi ambayo kipa wa Sudan hakuiona. Sio kipa wa Sudan tu, hata David de Gea asingefika. Jan Oblak asingefika. Manuel Neuer asingeokoa pia.

Bao la pili likafungwa na Nchimbi mwenyewe baada ya kazi nzuri ya Shaban Idd Chilunda. Furaha iliyoje. Lakini ghafla nikaanza kumuwaza Nchimbi.

Mpira wetu bwana. Huwa unafurahisha sana. Huyu Nchimbi mbona ana mlima na mabonde hivi?

Aliitwa timu ya taifa siku chache zilizopita. Sijui bahati mbaya au vipi lakini jioni yake alikuwa ameondoka na mpira Uwanja wa Taifa baada ya kuifunga Yanga hat-trick katika sare ya mabao 3-3 dhidi ya timu yake ya Polisi Tanzania.

Watu walihoji. Kwanini aitwe timu ya taifa kwa sababu ya kuifunga Yanga tu? Hakuonwa kabla ya hapo? Nadhani Kocha Msaidizi wa Taifa Stars, Suleiman Matola anamuamini kwa sababu ni mshambuliaji wake katika klabu ya Polisi Tanzania. Anajua kiwango chake.

Picha waliyomtengenezea Nchimbi haikuwa nzuri. Kwa wanaomfahamu wanadai alistahili kuitwa kabla ya kuipiga Yanga hat-trick. Hii inamaanisha kwamba kama angechemsha katika mechi za timu ya taifa mashabiki wangemuandama kuwa aliitwa kwa sababu ya ngekewa tu ya kuifunga Yanga lakini sio mchezaji mahiri. Walimuongezea presha isiyo na msingi.

Lakini hapohapo inashangaza kidogo. Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa, Etienne Ndayiragije ni mtu makini. Mpaka ninapoandika sasa hivi ni kocha wa Azam. Nasikia jana TFF ilikuwa mbioni kumpa timu hiyo moja kwa moja halafu Azam anapewa kocha mwingine. Unajiuliza, kwanini kocha wa Stars hakumuamini Nchimbi akiwa naye Azam kiasi kwamba alimpeleka kwa mkopo Polisi Tanzania. Labda sio yeye ndiye ambaye alifanya uamuzi hayo. Mpira wetu bwana!

Baada ya hapo unawaza bahati aliyonayo Nchimbi. Aliitwa katika dakika za mwishomwisho kuelekea Sudan kuchukua nafasi ya mtu. Ilikuaje akaanza mechi ya Sudan? Inaaminika kwamba mchezaji aliyeitwa kama nyongeza baada ya mwingine kuumia, basi hana nafasi sana. Ilikuaje akaenda na akaanza?

Kilichofurahisha zaidi ni kwamba akafunga bao la ushindi kabisa.

Ujumbe kwa wachezaji wetu kutoka kwa Nchimbi ni kwamba inabidi wapambane. Wapige kazi yao. Majungu na fitina wawaachie wahusika wengine. Mpira unajionyesha uwanjani. Nadhani kwa upande mwingine hiki ndicho pia alichokifanya Juma Kaseja.

Wachezaji wetu wanapitia katika milima na mabonde lakini wana nafasi ya kuibuka mashujaa. Na sasa baada ya kumalizika kwa msimu huu unaweza kusikia Simba au Yanga wanamchukua Nchimbi. Kuna wachezaji wengi waliwahi kuondoka timu kubwa wakarudi timu kubwa.

Lakini hauwezi kujua, unaweza kusikia Nchimbi amepata dili katika timu moja kubwa Sudan. Lakini pia hauwezi kujua. Ameshakuwa mchezaji muhimu kikosini. Mwakani kuna michuano ya Chan pale Cameroon na anaweza kujikuta amekwenda na kucheza vema na kupata timu nzuri nje ya nchi.

Wakati mwingine mchezo wa soka unashangaza kidogo. Una mabonde na milima halafu ghafla unatokea mteremko. Nahisi inaweza kuwa hivyo kwa Ditram Nchimbi.

Tukiachana na suala la Nchimbi nadhani wakati umefika kwa watu wa TFF kuliamini benchi la ufundi. Kuanzia kwa kocha mkuu na wasaidizi wake, Suleiman Matola na Juma Mgunda. Inaonekana wanawajua wachezaji wetu na ndio maana kazi yao inakuwa rahisi.

Jinsi Matola alivyomuingiza Nchimbi katika timu. Jinsi Mgunda alivyomuamini beki wa kati wa timu yake ya Coastal Union, Bakari Nondo ambaye alicheza sambamba na Nyoni katika safu ya ulinzi juzi. Lakini pia kocha mkuu ndiye ambaye ameendelea kumuamini Juma Kaseja ambaye alikuwa kipa wake katika klabu ya KMC kabla hajaenda Azam.