Hii kali Mourinho hakumtaka Fred Manchester United

Muktasari:

Man United ilitumia Pauni 52 milioni kunasa saini ya Mbrazili huyo, lakini Mourinho hakuwa na ujanja zaidi ya kukubali tu kwa sababu alihofia huenda Ed Woodward asingetua pesa kunasa kiungo mwingine aliyekuwa akimhitaji kwenye timu.

MANCHESTER, ENGLAND. HABARI ndiyo hiyo. Jose Mourinho hakutaka kabisa usajili wa kiungo wa Kibrazili, Fred asajiliwe na Manchester United alipokuwa kocha wa timu hiyo, lakini alikubali kwa sababu ya hofu kwamba timu isingenunua mtu kabisa.
Man United ilitumia Pauni 52 milioni kunasa saini ya Mbrazili huyo, lakini Mourinho hakuwa na ujanja zaidi ya kukubali tu kwa sababu alihofia huenda Ed Woodward asingetua pesa kunasa kiungo mwingine aliyekuwa akimhitaji kwenye timu.
Fred, 26, ameshinndwa kuonyesha makali yake tangu alipojiunga na timu hiyo akitokea Shakhtar Donetsk mwaka jana 2018. Mourinho alikuwa na wasiwasi kwamba Fed asingekuwa na uwezo wa kufanya vizuri kwenye klabu hiyo, lakini ambalo ndilo linalotokea kwa sasa.
Alimchezesha mara moja tu katika mechi sita za mwisho za kocha Mourinho kabla ya kufutwa kazi huko Old Trafford, lakini ameshindwa kupenya pia na kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha kocha Ole Gunnar Solskjaer.
Lakini, kocha Ole bado anaamini kwamba Fred anaweza kubadili mambo na kuwa mchezaji muhimu kikosini, akisema: “Ndio, sishangai kuona mchezaji wa kutoka Ukraine annapata shida kidogo mwanzoni mwa maisha yake England.
“Lakini, kuhusu kipaji anacho, tumeona kile ambacho Fred anaweza kutupatia kama kwenye ile mechi ya PSG, Arsenal na Man City. Naamini kuna kitu kikubwa atakifanya katika msimu huu.”