Mourinho amtaja Ronaldo, awatosa CR7, Messi

Muktasari:

Mreno huyo kwanza alikuwa mkalimani kwenye kikosi cha Barcelona, kipindi hicho Ronaldo akiwa na umri wa miaka 19 tu, akicheza kwenye timu hiyo, ambapo alifunga mabao 47 katika mechi 49.

London, England. KOCHA, Jose Mourinho amemtaja staa wa Brazil, Ronaldo kuwa mchezaji bora zaidi aliyewahi kumwona kwenye maisha yake ndani ya mchezaji huo, akiwapiga chini Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.
Kocha huyo wa zamani wa Chelsea, Manchester United, Real Madrid na Inter Milan amefanya kazi na mastaa wengi mahiri katika kipindi chake cha ukocha na kubeba mataji kibao makubwa.
Mreno huyo kwanza alikuwa mkalimani kwenye kikosi cha Barcelona, kipindi hicho Ronaldo akiwa na umri wa miaka 19 tu, akicheza kwenye timu hiyo, ambapo alifunga mabao 47 katika mechi 49.
Kisha Mbrazili huyo alikwenda kuonyesha ubora mkubwa kwenye vikosi vya Inter Milan, Real Madrid, AC Milan na Corinthians.
Mourinho alisema: "Ronaldo, El Fenomeno, Cristiano Ronaldo na Leo Messi wamekuwa na maisha marefu kwenye soka, kwa sababu wamethubutu kulinda viwango vyao kuwa bora kila siku kwa zaidi ya miaka 15.
"Hata hivyo, ukitazama vipaji na akili ya mpira ndani ya uwanja, hakuna anayemzidi Ronaldo (Nazario). Nilipokuwa Barcelona na Bobby Robson, hapo ndipo nilipomwelewa Ronaldo kuwa ni mchezaji bora zaidi kuwahi kumwona ndani ya uwanja.
“Majeruhi yalimuua mapema, lakini kile kiwango alichokionyesha kipindi kile akiwa na umri wa miaka 19, kilikuwa balaa.”
Mourinho aliwahi kufanya kazi na Cristiano Ronaldo kati ya 2010 na 2013 huko Real Madrid, ambako alikuwa akichuana vikali na Messi akiwa na chama lake la Barcelona na kuvunja utawala mwa wababe hao wa Nou Camp kwa kubeba taji la La Liga mwaka 2012.
Ronaldo wa Brazil amefunga mabao 414 katika maisha yake ya soka kwenye klabu na timu ya taifa.