Tanzania ‘Taifa Queens’ kuanza na Zambia netiboli Afrika

Muktasari:

Mara ya mwisho Tanzania ‘Taifa Queens’ ilitwaa medali ya fedha kwenye michezo ya Afrika nchini Msumbiji baada ya kufungwa na Uganda katika fainali kwa tofauti ya goli moja, wakati huo Tanzania ikiwa ya tatu katika viwango vya ubora Afrika.

Dar es Salaam.Timu ya Taifa ya Tanzania ya netiboli (Taifa Queens) itafungua dimba na Zambia katika mashindano ya Afrika yaliyopangwa kuanza Oktoba 18 hadi 22 nchini Afrika Kusini.

Taifa Queens inashiriki mashindano hayo baada ya kutoshiriki mashindano ya kimataifa kwa zaidi ya miaka sita mfululizo.

Msimu huu timu hiyo imerejea upya katika ushindani wa kimataifa na tayari Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta) kimewaita kambini wachezaji 30 kujiandaa na mashindano hayo.

Shirikisho la Netiboli Afrika, limetoa ratiba ambapo Tanzania iliyopo kundi A itafungua dimba na Zambia kabla ya kukukutana na wenyeji Afrika Kusini, Malawi na Lesotho.

Kundi hilo lina timu ngumu kulinganisha na kundi B lenye timu za Uganda, Zimbabwe, Kenya na Eswatin.

Kocha wa Taifa Queens, Argentina Daudi amesema licha ya kutoshiriki mashindano ya kimataifa kwa muda mrefu, lakini hana wasiwasi na ushiriki wao.

Awali Chaneta ilikuwa katika hatihati ya kushiriki katika mashindano hayo ambayo ni muhimu kuuweka mchezo wa netiboli katika orodha ya viwango vya dunia vinaandaliwa na Sshiriksiho la mchezo huo, IFN.

Mwenyekiti wa Chaneta, Devotha Marwa alisema kuwa BMT imelipia Dola 550 (SH1.3 milioni) na hivyo kuifanya Tanzania kupitishwa kushiriki katika mashindano hayo makubwa ya mchezo huo.

Marwa alisema kuwa kwa sasa wanasotea fedha ya kuiandaa timu ambazo ni Sh 104 milioni ambaoz bado hawajazipata pamoja na mashindano hayo kubakiza siku 17 kuanza.

“Tunaishukuru serikali kwa kuokoa ushiriki wetu, maana tulikuwa tunarejea kule kule tulipokikuta chama ambacho miaka sita hakikuweza kushiriki mashindano ya kimataifa na kufutiwa uwanachama wake,” alisema Marwa.

Alisema kuwa bado wapo katika mzigo mzito wa kuiwezesha timu ya Taifa kusafiri na kushindana mjini Cape Town.

“Tunawaomba wadau kutusaidia, kwani hii timu ni ya Taifa na inawakilisha nchi kama ilivyo Taifa Stars kwa upande wa mpira wa miguu,” alisema.

Alisema kuwa wachezaji wa timu ya Taifa kwa sasa wapo katika mazoezi chini ya kocha wao, Argentina Daudi.

Wachezaji hao ni  Mwanaidi Hassan, Lilian Jovin, Christina Kabendera, Asha Said,  Fatuma Machenga  ambao wanacheza nafasi  ya  ufungaji  (GS) huku  Kulwa Ased (GA), Evodia Kazinja, Elizabeth Fusi, Sarah Nakiyung na Sophia Komba (WA).

Wengine ni Gloria Benjamin, Angle Allan (C), Jesca Kimaro, Impala Iddi, Semeni Abeid, Faraja Malaki  na Lulu Misana (WD), Sekela Dominick, Merciana Samwel, Lilian Silidion (GD)  na  Rehema Juma na  Monica Aloi ni GK.