Yanga yafanya umafia Zambia, Zesco presha tupu

Thursday September 26 2019

Yanga yafanya, umafia Zambia, Zesco presha tupu, Mwanaspoti, Tanzania, soka

 

By KHATIMU NAHEKA

YANGA tayari iko Zambia tayari kwa vita ya marudiano na kumalizana dhidi ya Zesco United ya Zambia, lakini ilipotua ikashtukia kitu na kufumua ratiba kamili na ghafla tu ikaamua kutimkia Ndola kuwashtukiza wenyewe wao watakaovaana nao katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika keshokutwa Jumamosi.
Wawakilishi hao wa Tanzania wanatarajia kurudiana na Zesco  inayoonolewa na Kocha George Lwandamina kwenye mechi ya kuwania kutinga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya sare ya 1-1 nyumbani wiki mbili zilizopita.
Awali, mabosi wa Yanga akiwamo kocha wake mkuu, Mwinyi Zahera walipanga safari yao kuanza Jumatatu ya wiki hii lakini wakabadilisha na kuondoka siku moja baadaye kutokana na mabadiliko la ratiba ya safari ya ndege waliyotaka kuitumia, pia, walipanga kuweka kambi fupi jijini Lusaka kwa siku chache kabla ya kwenda Ndola ambapo mchezo huo utapigwa kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa.
Hata hivyo, jana Jumatano asubuhi Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Rodgers Gumbo alilithibitishia Mwanaspoti kuwa mpango wao huo umebadilishwa ghafla na  benchi la ufundi chini ya Kocha Zahera na kuamua kutimka Lusaka kwenda Ndola tofauti na mipango yao ya awali, jambo ambalo linaweza kuwashtukiza Zesco ambao kupitia kocha wake, George Lwandamina walikuwa wakifahamu kama wapinzani wao wameshatua Zambia, lakini watajichimbia kwanza Lusaka.
Gumbo alisema Kocha Zahera mara baada ya kutua jijini Lusaka na kugundua kuwa licha ya jiji hilo kuwa na baridi kidogo, lakini huko Ndola baridi lake limezidi kidogo na inaweza kuwasumbua vijana wake, haraka aliwataka mabosi wake kuiwahisha timu Ndola kuzoea mazingira kabla ya kuvaana na wenyeji wao.
Katika mpango huo, Zahera alikitaka kikosi chake kikafanye mazoezi ya kwanza Ndola jana Jumatano jioni kisha leo Alhamisi na kumalizia kesho Ijumaa ambapo watafanyia katika uwanja utakaotumika kwa mchezo wa Levy Mwanawasa kabla ya kushuka uwanjani Jumamosi Septemba 28.
“Tulikuwa na akili hiyo ya kuweka kambi pale Lusaka, lakini timu ilipofika kuna mambo yamelazimika kubadilishwa kidogo na haraka na ni maamuzi ya benchi la ufundi ambalo limetaka mabadiliko hayo,” alisema Gumbo ambaye jana jioni alianza safari ya kwenda Zambia kuungana na timu hiyo.
“Kuna baridi kidogo pale Lusaka, lakini pia kwa kuwa tulishatanguliza wenzetu kule Ndola kabla ya timu kufika wakakabidhi ripoti kwa makocha nao wakaona bora timu itangulie haraka kule na safari hiyo imeanza leo asubuhi (jana) na jioni yake wafanye mazoezi huko Ndola.
“Kusafiri pale umbali wake ni kama saa tano na njia ni salama kabisa tupo makini sana kuhakikisha tunapata kile tunachotaka katika mechi hii ya marudiano dhidi ya Zesco.”
Gumbo alisema mpaka sasa wachezaji wote waliopo kwenye msafara huo wanaendelea vyema na wana ari kubwa ya mchezo, wakijua ndio utakaoamua hatma ya timu yao kama itinge makundi ama itupwe kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ili kuwania kucheza makundi kama ilivyowahi kufanya mwaka 2016 na 2018.

MAMILIONI YAPUKUTISHWA
Taarifa zaidi kutoka ndani ya Yanga, zinasema mabosi wa klabu hiyo wametenga bajeti kamili kukamilisha safari yao hiyo ya ugenini kwa kiasi kisichopungua Sh 70 milioni kitatumika katika mchezo huo tu wa marudiano.
Gharama hizo ni zinazohusu malazi na chakula kwa siku zote watakazokuwa Zambia kabla ya kurejea jijini Dar es Salaam kuendelea na Ligi Kuu Bara.
Hata hivyo, imekuwa ngumu kufahamika mchanganuo mzima wa gharama hizo hasa baada ya kubadilishwa kwa makazi ya klabu hiyo, hata hivyo gharama halisi imekadiriwa si chini ya kiwango hicho hadi timu itakaporejea nchini.
Yanga kwenye mchezo huo dhidi ya Zesco inahitaji kupindua meza kwa kushinda ugenini ama kutoka sare inayoanzia mabao mawili ili kufuzu makundi la sivyo inaweza kuangukia kwenye playoff ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Hata hivyo, Yanga ina kazi kubwa kulingana na rekodi ya wenyeji wao kwenye Uwanja  huo wa  Levy Mwanawasa ambao huwa unawapa matokeo ya kuvutia.
Lakini  matokeo ya mchezo uliopita wa ligi hiyo  dhidid ya Township Rollers ya Botswana mjini Gaborone, yamekuwa yakiipa jeuri Yanga kwa kuamini inaweza kufanya chochote ugenini na kupenya kiulaini hatua inayofuata.

Advertisement