Ronaldo, Messi, Salah waongoza mastaa alioanza vibaya Ulaya

Thursday September 19 2019

Ronaldo, Messi, Salah waongoza, Mwanaspoti, Tanzania, mastaa kuanza, vibaya Ulaya

 

London, England.Wakati raundi ya kwanza ya hatua ya makundi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ikikamilika jana usiku, kundi kubwa la washambuliaji mastaa wametoka patupu huku nyota wasio na majina makubwa wakitamba.

Idadi kuba ya mastaa hao wamejikuta wakishindwa kufumania nyavu licha ya wengi kuwa na matarajio makubwa kwao kutamba katika mechi hizo za kwanza.

Dalili ya nyota hao kushndwa kufurukuta zilianza kuonekana kwenye mchezo baina ya Napoli na Liverpool ambapo Mohamed Salah na Sadio Mane walishindwa kuziona nyavu na kupelekea timu yao Liverpool kupoteza kwa mabao 2-0.

Huko Italia, Romelu Lukaku aliondoka patupu wakati klabu yake Inter ilipolazimishwa sare ya bao 1-1 na Slavia Prague, bao la wenyeji likifungwa na Nicolo Barella huku wageni wakifunga kupitia Peter Olayinka

Safu inayotajwa kuwa bora ya ushambuliaji duniani kwa sasa ya Barcelona inayoundwa na Lionel Messi, Antoine Griezman na Luis Suarez, ilishindwa kufua dafu mbele ya safu ya ulinzi ya Borussia Dortmund baada ya timu hizo kutoka sare ya bila kufungana juzi.

Kwenye mechi hiyo, Messi aliingia kutokea benchi dakika ya 59 akichukua nafasi ya Anssumane Fati.

Advertisement

Jijini Paris, Ufaransa jana, Eden Hazard, Gareth Bale, Luka Jovic na Karim Benzema walishindwa kuwa na msaada kwa Real Madrid ambayo ilijikuta ikichapwamabao 3-0 na wenyeji PSG.

Hata hivyo Bale ambaye amekuwa sio kipenzi cha kocha Zinedine Zidane, kwenye mechi hiyo alifunga bao ambalo lilikataliwa mnamo dakika ya 35.

Hali ilikuwa tete pia kwa Cristiano Ronaldo ambaye licha ya timu yake Juventus kulazimisha sare ya mabao 2-2 ugenini dhidi ya Atletico Madrid, alishindwa kufumania nyavu huku Blaise Matuidi na Juan Cuadrado wakifunga upande wa 'Bibi Kizee wa Turin'

Lakini mambo yamewanyookea Angel Di Maria, Robert Lewandowski, Harry Kane, Lucas Moura, Ryad Mahrez,Gabriel Jesus na Dries Mertens ambao waliweza kuzifungia mabao timu zao za Napoli, Manchester City, Tottenham Hotspurs, Bayern Munchen na PSG kwenye raundi hiyo ya kwanza.

Wakati idadi kubwa ya mastaa ikishindwa kufua dafu, mechi hizo za kwanza zimegeuka neema kwa baadhi ya wachezaji ambao hawana majina makubwa waliotamba kwa kupachikia mabao timu zao.

Jina la kinda Erling Braut Haaland wa Red Bull Salzburg ndio limetikisa zaidi baada ya kupachika mabao matatu kwenye mechi yao dhidi ya Genk huku wakifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 6-2.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 19 ni mtoto wa nyota wa zamani wa Norway na klabu za Manchester City, Nottingham Forest na Leeds United, Alf-Inge Håland.

Mwingine ni nyota wa Dinamo Zagreb, Mislav Orsic ambaye naye alifunga mabao matatu 'hat trick' kwenye mchezo wa timu yake dhidi ya Atalanta ambao waliibuka na ushindi wa mabao 4-0.

Advertisement