Lampard amtetea Barkley kwa kukosa penalti, Chelsea ikilala nyumbani

Muktasari:

Lawama nyingi zimekuwa zikielekezwa kwa Barkley kwa kung’ang’ania kupiga penalti hiyo huku akiwa sio chaguo la kwanza wala la pili la Chelsea katika upigaji wa penalti

London, England. Kocha wa Chelsea, Frank Lampard amemtetea mchezaji wake Ross Barkley kwa kuwa ni miongoni mwa wapigaji penalti wa timu hiyo baada ya kiungo huyo kukosa penalti dhidi ya Valencia jana usiku.

Kitendo cha kukosa penalti hiyo kiliinyima nafasi Chelsea kusawazisha na kujikuta ikichapwa bao 1-0 nyumbani kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.

Lawama nyingi zimekuwa zikielekezwa kwa Barkley kwa kung’ang’ania kupiga penalti hiyo huku akiwa sio chaguo la kwanza wala la pili la Chelsea katika upigaji wa penalti, lakini Lampard ameamua kusimama na nyota wake na kudai kuwa hakuna tatizo.

“Ross ni mpigaji wa penalti. Amefunga mechi kadhaa za maandalizi ya msimu na leo (jana) ilikuwa apige wakati alipoingia na akakosa. Sijui majadiliano yalikuaje. Jorginho na Willian walikuwa ni wapigaji penalti ndani ya uwanja na Barkley alipoingia naye akawa mpigaji penalti  na akakosa,” alisema Lampard.

Hata hivyo, kocha huyo amedai kuwa walikuwa na nafasi ya kupata ushindi kwenye mchezo huo pasipo kutegemea penalti hiyo, lakini walishindwa kutumia vizuri nafasi walizopata.

“Tulipaswa kushinda au hata kutoka sare. Tulitengeneza nafasi za kutosha na pia tulipata penati na tulijikuta tukiruhusu bao kwa shuti lao moja tu lililolenga lango,” alisisitiza Lampard.