Ndayiragije ajipa matumaini ya kushinda ugenini Zimbabwe

Mshambuliaji wa Azam, Obrey Chirwa akipiga shuti wakati wa mchezo dhidi ya Triangle United ya Zimbabwe. Azam ilifungwa bao 1-0. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

Pamoja na Azam FC kujiwekea mlima mrefu kwenye mechi ya marudiano na Triangle FC ya Zimbabwe baada ya kupigwa nyumbani bao 1-0, kocha wa timu hiyo haimsumbui anaamini atashinda ugenini.

Dar es Salaam. Kocha wa Azam FC, Etienne Ndayiragije amesema pamoja na kupoteza mechi nyumbani dhidi ya Triangle United ya Zimbabwe hajakata tamaa ya kusonga mbele katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Azam FC imecheza hatua ya pili ya mashindano hayo baada ya kuwaengua Fasil Kenema ya Ethiopia, ugenini walifungwa bao 1-0, Chamazi walishinda 3-1.

Katika mchezo wao wa jana Jumapili uliocheza Uwanja wa Azam Complex, Azam FC ilipigwa bao 1-0 na Triangle, hilo halijaonekana kumtisha Ndayiragije ambaye ametamka kauli ya kijasiri kwamba mpira ni dakika 90.

Ndayiragije alisema kama wameweza kufungwa uwanja wa nyumbani na wao wanaweza wakawashinda wapinzani wao ugenini, akisisitiza hawana presha na hilo.

"Kwanza wao ndio watakuwa na presha na sisi na sio sisi kuwa na presha na wao, tumejipanga tupo tayari kwa ajili ya kusaka nafasi ya kusonga mbele"

"Haitakuwa mechi rahisi, lakini tupo kwa ajili ya kupambana, asikuambie mtu mpira ni dakika 90 ndizo zinakuwa zinaamua kabla ya hapo hakuna anayekuwa anajua anavuna nini, tuna nafasi kwa sehemu nimeona wapinzani wetu walivyo," alisema Mrundi huyo.