Hizo Simba, Yanga zitachomokea hapa Ligi ya Mabingwa Afrika

Monday August 19 2019

Hizo Mwanasport, Simba, Yanga zitachomokea hapa, Mwanaspoti, Michezo, Tanzania

 

By CHARLES ABEL

Dar es Salaam. WAWAKILISHi wa Tanzania katika mechi za kimataifa msimu huu, Simba, Yanga, Azam, KMC, KMKM na Malindi zina kibarua kigumu cha kuhakikisha zinashinda mechi za marudiano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika ili zisonge mbele kwenye michuano hiyo.
Timu hizo zinatarajiwa kurudiana na wapinzani wao kwenye michuano hiyo ya CAF wikiendi hii, timu tatu za Simba, Azam na KMC zikiwa nyumbani na Yanga wakienda ugenini kama ilivyo kwa KMKM na Malindi za Zanzibar.
Katika mechi zao za kwanza timu hizo hazikupata matokeo mazuri ya kuwaweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele, kwani Simba ilitoka suluhu ugenini dhidi ya UD Songo ya Msumbiji kama ilivyokuwa kwa KMC ilipoumana na AS Kigali katika Kombe la Shirikisho.
Yanga ilitoka sare ya bao 1-1 nyumbani dhidi ya Township Rollers, Azam ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Fasil Kenema ya Ethiopia, KMKM ililala 2-0 dhidi ya Agosto ya Angola kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar huku Malindi ikilazimisha sare ya 0-0 ugenini dhidi ya Mogadishu City ya Somalia.
Udhaifu uliozigharimu timu hizo za Tanzania kwenye mechi za kwanza ni kuyumba kwa safu zao za ulinzi, pia ubutu upande wa ushambuliaji uliwaangusha.
Kwa ujumla, timu hizo sita za Tanzania zilifunga bao moja tu kwenye mechi zao za awali tena bao lenyewe likipatikana kwa mkwaju wa penalti, pale Patrick Sibomana alipotupia kambani akiisawazishia Yanga mbele ya Township waliofunga bao lao mapema.
Matokeo hayo ya mechi za mkondo wa kwanza yanazipa presha klabu hizo hasa Simba na Yanga kutokana na maandalizi makubwa ambayo zimefanya kabla ya msimu huu kuanza kwa kufanya usajili wa gharama na kuweka kambi zilizogharimu kiasi kikubwa cha fedha.
Hata hivyo, timu hizo licha ya matokeo ya mechi za kwanza kutokuwa mazuri kwao, bado zina nafasi ya kufanya vyema na kusonga mbele hatua inayofuata ya mashindano hayo na kwa kuliangalia hilo, makala hii inaainisha mambo matano ambayo yanaweza kuibeba kila timu kwenye mechi za marudiano ili ziweze kusonga mbele.

SIMBA
Kwanza Simba inapaswa kuhakikisha safu yake ya ulinzi haifanyi makosa ya mara kwa mara kama ilivyokuwa kwenye mechi ya kwanza ugenini ambayo yangeweza kuipatia mabao Songo kama washambuliaji wake wangekuwa makini.
Pili ni umakini na utulivu wa safu ya ushambuliaji katika kutumia nafasi lakini pia timu nzima kiujumla katika kuzitengeneza na tatu kinachoweza kuibeba Simba ni faida ya kucheza uwanja wa nyumbani.
Rekodi zinaonyesha Simba imepoteza mechi ya kimataifa nyumbani kwa mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2013 walipolala bao 1-0 dhidi ya Recreativo do Libolo ya Angola, rekodi ambayo inaweza kuiweka katika hali nzuri kisaikolojia kwa mchezo wao wa marudiano. Lakini pia kitu kingine kinachoweza kuwabeba ni rekodi isiyovutia ya wapinzani wao pindi wanapocheza ugenini.
UD Songo katika mechi nane za kimataifa walizocheza ugenini, hawajapata ushindi hata mara moja, wametoka sare mbili na wamefungwa mechi sita, wakifunga mabao matano na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara 15
Jambo la mwisho ni Simba kutumia mfumo wa 4-3-3 ambao utawajumuisha viungo wawili wa ushambuliaji ambao wataifanya itengeneze idadi kubwa ya nafasi za mabao na kufunga mabao mengi ambayo yanaweza kuivusha kwenda hatua inayofuata.
Hivyo kama Kocha Patrick Aussems na vijana wake watajiweka vyema na kujituma kama walivyofanya kwenye mechi yao ya Ngao ya Jamii iliyopigwa juzi usiku dhidi ya Azam FC ni wazi itapenya kiulaini kwa kuzingatia haijawahi kuwaangusha mashabiki wake Taifa.

YANGA
Yanga haikucheza vibaya dhidi ya Township kwenye mechi ya kwanza nyumbani ambayo iliisha kwa sare ya bao 1-1.
Mambo matano ambayo huenda yakaibeba Yanga ugenini mojawapo ni historia yake ya kupata ushindi ugenini dhidi ya timu za Kusini mwa Afrika ambayo inaweza kuwajenga vizuri kisaikolojia wachezaji wake.
Mfano wa timu za Kusini mwa Afrika zimewahi kuonja vipigo kutoka kwa Yanga wakiwa kwao, ni pamoja na  Komorozine ya Comoro na BDF XI ya Botswana.
Jambo la pili ni kuimarika kwa kikosi chake baada ya urejeo wa beki Kelvin Yondani na Juma Abdul kinaweza kuisaidia Yanga kuwa imara kwenye mchezo wa ugenini japo itaendelea kukosa huduma ya kipa Farouk Shikhalo.
Kingine ni mabadiliko ya kimfumo kwa kutumia ule ambao utaifanya itengeneze idadi kubwa ya nafasi na pia iwe na namba kubwa ya wachezaji kwenye safu ya ushambuliaji, ili kuilazimisha Rollers kucheza kwa kujilinda lakini cha nne ni kufunga bao la mapema ambalo litawaweka wapinzani wao kwenye presha.
Jambo la tano ambalo linaweza kuibeba Yanga ni kucheza mechi hiyo ikiwa haina presha kubwa ya mashabiki wake tofauti na inavyokuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Taifa jambo litakalowafanya wachezaji wacheze kwa utulivu wa hali ya juu na kutofanya makosa ya mara kwa mara.

AZAM, KMC, KMKM NA
MALINDI SASA
Faida ya kucheza nyumbani inaweza kuwa chachu kwa Azam na KMC kufanya vyema kwenye mechi za marudiano
Uimara wa safu zao za ushambuliaji katika kutumia nafasi ambazo kila timu itatengeneza na kujilinda vyema, itakuwa ni silaha kubwa kwa wawakilishi hao wawili wa Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho kufanya vyema.
Mabingwa wa Zanzibar KMKM wameanza vibaya na wana mtihani mkubwa wa kupindua magoli 2-0 ugenini. Njia bora kwao ni kucheza kwa kujichia na kujilinda kwa pamoja kwa sababu hawana cha kupoteza.
Malindi ina faida ya uwanja wa nyumbani. Ina kila sababu ya kusonga mbele. Kama iliwabana Mogadishu City kwao, inaweza kuwamaliza kwenye Uwanja wa Amaan.
KIKWAZO HAPA TU!
Kwa Simba, pamoja na Songo kutokuwa na rekodi ya kutopata ushindi ugenini, imekuwa ikifunga mabao hivyo kama safu yake ya ulinzi ya Wekundu wa Msimbazi ikizembea, wapinzani wao wanaweza kutumia mwanya huo kuwaadhibu.
Kwa Yanga wanapaswa kujipanga vilivyo kuikabili safu ya ulinzi ya Rollers ambayo huwa wagumu kuruhusu nyavu zake kutikiswa pindi inapokuwa nyumbani, kwani imefungwa mabao matatu tu kwenye mechi saba zilizopita, pia mabeki wa Yanga wanapaswa kucheza kwa tahadhari dhidi ya safu ya ushambuliaji ya wapinzani wao ambayo katika mechi saba za mwisho za kimataifa nyumbani imepachika mabao nane.
Azam, KMC, MKMK na Malindi kila moja inapaswa kujichunga na kutanguliwa kuruhusu mabao ya mapema ambayo yanaweza kuwaongezea presha na kuziweka kweye wakati mgumu katika mechi hizo.
Kiujumla kila timu inapaswa kujichunga na mipira ya adhabu na kona ambayo imekuwa changamoto kwa timu za Tanzania pindi zinapocheza mechi za kimataifa.

PRESHA MAKOCHA
Makocha wa timu zote, Aussems wa Simba, Mwinyi Zahera wa Yanga, Jackson Mayanja wa KMC na Etienne Ndaiyagije wa Azam kila moja kwa nyakati tofauti wamekuwa wakisisitiza kuwa, wapo tayari kupata matokeo kwenye mechi za marudiano.
Kocha wa Simba, Patrick Aussems, amesema, “Bado naamini hata sisi tuna nafasi ya kupata matokeo na kuwang’oa wapinzani wetu, kuna makosa madogo yaliyotugharimu, lakini tupo tayari kwa mchezo huo.Kikubwa hatujaruhusu bao la ugenini na tunamalizia nyumbani ambako tuna rekodi nzuri.”

Advertisement