Ambokile mambo yake safi TP Mazembe, Singano avuta pumzi

Muktasari:

TP Mazembe ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya DR Congo, watauanza msimu huu wa 2019/20 kwa kutupa karata yao ya kwanza nyumbani kucheza Jumanne dhidi ya Bukavu Dawa.

STRAIKA wa zamani wa Mbeya City, Eliud Ambokile amesema yupo tayari kuuanza msimu mpya wa Ligi Kuu DR Congo ‘Linafoot’  akiwa na TP Mazembe baada ya kupata leseni ya kucheza soka  la kulipwa.
TP Mazembe ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya DR Congo, watauanza msimu huu wa 2019/20 kwa kutupa karata yao ya kwanza nyumbani kucheza Jumanne dhidi ya Bukavu Dawa.
Ambokile mwenye umri wa miaka 25, alisema awali mchezo huo ulitakiwa uchezwe jana (Jumapili) lakini shirikisho la soka la Congo liliusogeza mbele hadi Jumanne.
“Natamani kupata nafasi ya kucheza kwenye mchezo wa kwanza wa msimu, nimekuwa na muda wa kutosha kujiandaa na huu msimu, najiona kuwa tayari lakini mwenye maamuzi ya  mwisho siku zote ni kocha,” alisema Ambokile.
Straika huyo, alisema huu unaweza kuwa msimu wake wa  mfanikio kwenye uchezaji wake wa soka kutokana na kutowahi kushinda kombe la Ligi Kuu kwenye uchezaji wake soka tangu akiwa Tanzania ambako alikuwa akiichezea Mbeya City.
“Naamini nitashinda makombe kwa kweli hiyo ni shauku ya kila mchezaji na sio peke yangu hasa anapokuwa kwenye timu kubwa,” alisema straika huyo.
SINGANO AVUTAPUMZI
Naye winga wa zamani wa Simba na Azam FC, Ramadhani Singano ‘Messi’aliyetua TP Mazembe amesema tayari ameshazoeana na wachezi wenzake kinachosubiriwa ni kuanza tu majukumu ya kuitumikia timu hiyo.
“Tumeshakuwa wenyeji ule ugeni umetutoka na nashukuru Mungu kwa kupatikana mapema kwa leseni zetu za kucheza soka nchini hapa,” alisema Singano.