Mfungaji bora Afrika kikapu hakamatiki RBA

Muktasari:

Savio ni bingwa mtetezi wa ligi hiyo kwa mara ya pili mfululizo, ingawa msimu huu anapewa presha ya kutetea ubingwa na JKT na Oilers.

Dar es Salaam. Unamkumbuka Baraka Sadiki Athuman? Yule mfungaji bora wa kikapu Afrika Mashariki na Kati aliyeiletea Tanzania tuzo kwenye mashindano yaliyofanyika Uganda.

Jamaa unaambiwa hakuna wa kumtoa kwenye reli katika Ligi ya Mpira wa Kikapu mkoa wa Dar es Salaam (RBA) iliyoingia mzunguko wa pili.

Baraka anayechezea JKT tayari amefunga mara 42 akimuacha mbali Erick Lugora wa Oilers ambaye anafuatia akiwa amefunga mara 29 sawa na Dominck Zacharia wa Kurasini Heat.

"Mazoezi ndiyo yananiongoza," anasema Baraka ambaye amekulia na kulelewa katika timu ya JKT tangu udogo wake mpaka sasa.

Wababe wengine, Harrison Banda wa Oilers, David Msitu wa Magnet na Emmanuel Mwendo wa Tanzania Prisons wanachuana kusaka tuzo ya mfungaji bora wa Ligi hiyo ambayo iko kwenye mzunguko wa lala salama.