Malinzi aieleza Mahakama jinsi anavyoidai TFF

Tuesday August 13 2019

 

By Fortune Francis

Dar es Salaam. Aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ameeleza mahakama kuwa siku chache kabla ya kukamatwa aliikopesha TFF Sh15 milioni na anaamini bado anaidai ingawa hana uwakika ni kiasi gani.

Malinzi alidai hayo leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati akitoa utetezi wake baada ya kukutwa na kesi ya kujibu.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo Katibu wake Celestine Mwesigwa, Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga na Karani Flora Rauya.

Akiongozwa na Wakili wa utetezi, Richard Royongeza mbele ya Hakimu Mkazi Maira Kasonde alidai fedha hizo zilikuwa ni kwaajili ya mchezo wa kwanza wa kufuzu fainali za Afrika kati ya Tanzania na Lesotho.

Alisema fedha hizo aliziingiza kwenye akaunti ya TFF kwenye benki ya Diamond Trust (DTB) ambapo ilikuwa kwaajili ya kurusha matangazo ya moja kwa moja wakati wa mchezo huo.

"Ilikuwa ni makubaliano ya mkataba kati ya kampuni ya bia ya Serengeti ambapo walitaka ili kudhamini mchezo huo matangazo ya mpira kurushwa moja kwa moja kupitia TBC," alidai Malinzi.

Advertisement

Akiendelea kujitetea Malinzi alidai wakati anaingia TFF alikuta changamoto kubwa ya kifedha ambapo ilikuwa ikidaiwa madeni makubwa na malaka ya mapato (TRA) na kuoelekea kuzifungia akaunti za shirikisho hilo.

"Nilipoingia zilikuwa zikija hati za Mahakama za kukamata mali za TFF wafanyakazi walilipwa mafao yao na kusainishwa mikataba ya muda kunusuru hali iliyokuwepo"

"2014 kampuni ya Yono ilipata kibali cha Mahakama cha kukamata basi la TFF kampuni hiyo ililikamata mchana na mimi nilitua fedha zangu mfukoni Sh20 milioni ili lkuachiwa" alidai

Aliendele kudai kama Rais alihakikisha shughuli mbalimbali za timu zinakwenda hadi kushiriki michuano mbalimbali ya kimataifa.

"Ili kunusuru hali hiyo ilikuwa ikinilazimu kutumia fedha zangu za mfukoni ili kuinusuru TFF hali ikiwa nzuri narudishiwa na wakati mwingine kukopa kwenye kamati tendaji na kwa watu binasfi," alidai

Malinzi alidai wapo mashahidi wa upande wa mashtaka waliodhibitisha jambo hilo Mahakamani akiwemo Katibu Mkuu Wilfred Kidao, Danieli Msangi, Hellen Adam na Sareki Yonasi.

Aliongeza pamoja na kuwa idara ya uhasibu ya TFF imekuwa ikitengeneza akaunti ikionyesha fedha alizokopesha na alizolipwa.

"Shahidi wa sita Danieli Msangi alidhibitisha kuwa na akaunti TFF na kuieleza Mahakama hadi kufikia Agosti 14, 2014 nilikuwa nikidai 130 milioni" alieleza

"Akaunti yangu ya TFF ipo na haijawahi kuletwa inaonyesha namna nilivyokuwa nakopesha na nilivyokuwa nalipwa."

Hakimu Kasonde aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 15 mwaka atakapokuja kutoa uamuzi wa kupokelewa kwa kielelezo cha nyaraka ya taarifa ya madeni kati ya TFF na Malinzi.

Katika kesi hiyo mashahidi 15 wa upande wa Mashtaka walitoa ushahidi katika akiwemo Katibu Mtendaji wa TFF Wilfred Kidao.

Kesi hiyo ya jinai namba 213 ya mwaka 2017 washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 20 yakiwamo ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha wa USD 173,335.

Malinzi, Mwesigwa na Nsiande wapo rumande kwa kukabiliwa na mashtaka ya utakatishaji wa fedha kuwa miongoni mwa mashtaka  ambayo kwa mujibu wa sheria hayana dhamana huku Frola akiwa nje kwa dhamana.

 

Advertisement