Manyika huyo kumrithi Pondamali, Yanga yajifua kinoma Moro

Thursday July 11 2019

Mwanaspoti, Manyika huyo, kumrithi Pondamali, Yanga yajifua, Morogoro, Mwanasport, Michezo

 

Dar es Salaam. Mabadiliko ndani ya benchi la ufundi la Yanga yameanza baada ya Peter Manyika ameonekana ameanza kazi rasmi akichukua nafasi ya Juma Pondamali ya kuwa kocha wa makipa.

Ingawa uongozi wa Yanga haujamtangaza Manyika, lakini mkongwe huyo jana alionekana akiwa mazoezini akiwafua makipa wa timu hiyo huku Pondamali hakuwepo mazoezini.

Yanga ilikuwa inapiga hesabu muda mrefu katika kufanya mabadiliko katika kitengo cha makipa wakidai Pondamali amepungua ubora kuwapa makali makipa wao.

Katika hatua nyingine Yanga imeendelea kufanya mazoezi makali wakiwa kambini Morogoro, lakini dozi kubwa ni wachezaji wanajazwa pumzi na stamina na mastaa wanakiona cha moto.

Kocha msaidizi Noel Mwandila aligawa kikosi hicho katika makundi mawili kisha kila kundi akalipa kitu chake maalum ndani ya uwanja huo wakitakiwa kukimbia bila kukutana wala kupishana.

Kundi la kwanza lilikuwa na Pappy Kabamba Tshishimbi, Patrick Sibomana, Issa Bigirimana, Lamine Moro, Jafary Mohamed, Gustavo Simon, Mohamed Issa na Paul Godfrey.

Advertisement

Kundi lingine Mwandila akawaweka straika Juma Balinya, Mustapha Seleman, Muharami Issa, Maybin Kalengo, Mapunduzi Balama, Abdulaziz Makame na Cleophas Sospeter.

Makundi hayo yalitumia saa moja na nusu wakikimbia mbio kwa kasi kubwa huku kila baada ya dakika tatu wakipumzika kwa kunyoosha viungo.

Katika mapumziko hayo Mwandila alionekana kuwa mkali akitaka kila mchezaji kunyoosha vikungo kwa kufanya mazoezi binafsi huku akipiga marufuku mtu kukaa wala kulala.

Hata hivyo, baada ya mazoezi hayo ya mbio wachezaji hao baadaye walibadilisha aina ya mazoezi na kuchezea mpira kidogo kisha baadaye kufunga mazoezi hayo ya asubuhi.

Advertisement