Ndugai afunguka wabunge kudaiwa kuidhihaki Stars

Muktasari:

Baada ya kiongozi mmoja wa Serikali kuwatuhumu baadhi ya wabunge kuwa wamewalaumu wachezaji na timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inayoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), Spika Job Ndugai amesema kiongozi huyo hajitambui na hajielewi

Dodoma. Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema kiongozi mmoja wa Serikali aliyezungumza maneno yasiyofaa kuhusu Bunge la Tanzania na wabunge na kumdanganya hadharani Rais John Magufuli kuwa wawakilishi hao wa wananchi wamewadhihaki wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, hajitambui.

Ndugai ametoa kauli hiyo leo Jumanne Juni 25, 2019 wakati akijibu mwongozo wa mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe aliyehoji kauli iliyotolewa na kiongozi huyo, akidai kuwa inalidhalilisha Bunge.

Zitto alitoa kauli hiyo baada ya Ndugai kabla ya wabunge kuanza kupiga kura kupitisha bajeti ya Serikali mwaka 2019/2020 ya Sh31 trilioni, kusema kati ya wabunge waliokwenda Misri ambako timu ya Taifa inashiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), hakuna aliyemlaumu mchezaji yeyote wala kuisema vibaya timu hiyo.

Baada ya kauli hiyo Zitto aliomba mwongozo, “Kwa mujibu wa kanuni ya 68 (7) kuhusu jambo lililotokea bungeni mapema naomba kupata ufafanuzi wako, muda mfupi uliopita umeeleza jambo lililotokea nje ya Bunge ambapo mmoja wa viongozi wa Serikali mbele ya kiongozi mkuu wa nchi amewabagaza wabunge ukiwemo wewe mwenyewe.”

“Lakini maelezo uliyotoa utadhani sio mkuu wa mhimili, umetoa maelezo kama unajitetea mbele ya kiongozi huyo kitu ambacho nadhani Spika tunapaswa kupata mwongozo wako, maana atatokea mwingine atawasema wabunge na hakutakuwa na chochote cha kufanywa,” alisema Zitto.

Ameongeza, “Wewe hauruhusu mhimili wa Bunge kuchezewa, kutomaswa na kudharauliwa nini kilichokupata leo unasamehe kabla ya kuchukua hatua yoyote. Simama kulinda hadhi ya Bunge na wabunge hawajawasema wachezaji

Katika majibu yake Ndugai amesema, “Hayo ni mawazo ya mtu ambaye kidogo ndio hivyo. Ni bahati mbaya sana tuna viongozi wa Serikali wanadiriki kumdanganya Rais hadharani, kiongozi wa Serikali unapoongea mbele ya rais jipange uongea ukweli mtupu wa mwenyezi Mungu, usisingizie wala kumuonea mtu hatufanyi hivyo.”

“Natamani ningefunguka kidogo kuhusu…, bahati mbaya kijana wetu huyu hajitambui na hajielewi na kwasababu ana nguvu aliyonayo ana makundi ya vijana kwenye mitandao anaweza kumtukana Spika, kuwasingizia wabunge wamekosa nini? Kama kuna mtu ana deni la kufanya kidogo kuhusu hao wachezaji basi ni yeye. Akitaka niseme ila kwa leo inatosha.”