Raila kuongoza mashabiki kuishangalia Harambee Stars dhidi ya Algeria

Sunday June 23 2019

Mwanasport, Raila kuongoza mashabiki, kuishangalia Harambee Stars dhidi ya Algeria, Mwanaspoti, Michezo blog

 

By Fadhili Athumani

Cairo, Misri. Waziri mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga atawaongoza mashabiki wa Kenya kuishangilia Harambee Stars itakaposhuka dimbani leo, kuanzia saa tano, kuwakabili Algeria katika mchezo wa Kundi C wa fainali za Mataifa ya Afrika.

Raila Odinga anaongoza msafara wa viongozi wa ngazi za Juu za Serikali alitua Jijini Cairo Alhamisi Juni 20, aliwatembelea wachezaji katika hoteli waliyofikia Jijini Cairo, akiwa na ujumbe kutoka kwa timu hiyo, iliyofuzu kushiriki fainali hizi, kwa mara ya kwanza baada ya miaka 15.

Akizungumza na wachezaji alipowatembelea, Raila aliyeongozana na Waziri wa Ugatuzi, Eugene Wamalwa na Balozi wa Kenya nchini Misri, Joff Otieno aliwataka wachezaji kujituma uwanjani huku wakitambua kwamba Wakenya wako nyuma yao.

“Nimevutiwa sana na maandalizi yaliyofanyika mpaka sasa, niwahahakikishie tu kwamba, Wakenya wako nyuma yenu, Rais Kenyatta amenituma kuwahakikishia sapoti yake," alisema Raila.

Aidha, Raila aliwataka Wakenya kujitokeza kwa wingi kuisapoti Stars, kwa kutuma jumbe za hamasa na ikiwezekana kujaza uwanja wa Jeshi wa Cairo, timu itakapoivaa Algeria leo.

Kauli ya Raila, inaungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake, William Ruto ambao kwa pamoja wamerekodi video fupi ya hamasa kwa Stars, na kutupia kwenye mitandao ya jamii na kituo cha taifa cha KBC, ambayo inaonesha mechi zote 52.

Advertisement

Nahodha wa Harambee Stars, Victor Wanyama, aliishukuru Serikali kwa kuhakikisha timu inapata kila kitu ikiwemo kulipa posho kwa wakati, jambo ambalo limeongeza morali kikosini.

“Tunaishukuru sana Serikali na Wakenya kwa sapoti kubwa waliotupa tangu tuingie kambini Ufaransa, hatuna cha kuwalipa zaidi ya kujituma uwanjani na kupata matokeo chanya, hatutawaangusha," alisema Wanyama.

Wanyama, anayekipiga katika klabu ya Tottenham Hotspur ya England, alisema wako tayari kwa ajili ya mechi ya leo, huku akiwataka Wakenya kuwaamini na kuendelea kuwapa sapoti hasa katika mchezo wa leo.

Harambee Stars, ambayo imepangwa katika kundi C, itatupa karata yake ya kwanza leo kabla ya kuivaa Taifa Stars ya Tanzania (Juni 27), kisha itamaliza kampeni yake kwenye kundi lao dhidi ya Senegal, Julai Mosi. Mechi zote zitapigwa kwenye uwanja wa Jeshi, maarufu Cairo June 30 (Air Defence) Stadium, yenye uwezo wa kuingiza mashabiki 30,000.

Advertisement