VIDEO: Taifa Stars yahama hoteli tayari kwa Afcon, kuivaa Zimbabwe leo

Muktasari:

Vijana hao wa Amunike ambao kwenye mchezo uliopita wa kirafiki walipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya wenyeji wa fainali hizo, Misri wamepangwa kundi C kwenye AFCON na timu za mataifa ya Algeria, Senegal na Kenya.

Cairo, Misri. Timu ya Taifa ya Tanzania “Taifa Stars” imeripoti rasmi kwenye Hoteli ya Helnan Landmark, New Cairo watakayokuwa wakikaa kwa muda wote wa mashindano ya Mataifa ya Afrika (Afcon).

Taifa Stars ilikuwa kambini Misri kwa zaidi ya wiki sasa, lakini ilikuwa katika hoteli waliyokodi wenyewe nje ya utaratibu wa CAF.

Taifa Stars ilipokelewa hotelini na ngoma za asili ya Misri huku wachezaji wakionekana kufurahi mazingira ya hotel hiyo.

Vijana hao wa Emmanuel Amunike walipata muda wa kupumzika kidogo na kabla ya mchezo wao wa kirafiki dhidi ya Zimbabwe utakaochezwa saa 2.00 usiku kwenye uwanja wa mazoezi wa Maadi Olympic Centre, Cairo.

Hii ni mechi ya pili na mwisho wa kirafiki kwa Stars kabla ya Afcon itakayoanza Juni 21 hadi Julai 19, baada ya ule wa Jumatano iliyopita dhidi ya Misri ambao ilifungwa bao 1-0.

Kocha wa Stars, Emmanuel Amunike alisema ana imani kubwa mechi za kirafiki zitawasaidia kufanya vyema kwenye kundi lao la C pamoja na Algeria, Senegal na Kenya.

Amunike alisema lengo lake ni kuivusha Taifa Stars katika hatua ya makundi ya fainali za mataifa ya Afrika ‘AFCON’ nchini Misri, zitakazoanza kuchezwa mwezi huu.

Vijana hao wa Amunike ambao kwenye mchezo uliopita wa kirafiki walipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya wenyeji wa fainali hizo, Misri.

 “Tulicheza kwa kuziba nafasi dhidi ya Misri kwa kiasi kikubwa tulifanikiwa. Lengo letu ni kuimarika kwa kiango chetu kadri itakavyowezekana,” alisema mchezaji huyo wa zamani wa FC Barcelona.

“Kiukweli tumepangwa kundi gumu lakini tutafanya kila litakalokuwa ndani ya uwezo wetu tuvuke katika hatua ya mkundi kwa kuingia raundi iliyofuata.

“Sidhani kama Senegal watakuwa dhaifu bila ya Mane, ni mchezaji mzuri lakini wanao wachezaji wengine wazuri na wanapewa nafasi kubwa,” alisema Amunike.

Amunike ambaye anakinoa kikosi cha Taifa Stars, aliisaidia timu yake ya taifa ya Nigeria kutwaa ubingwa wa AFCON mwaka 1994 kipindi hicho akiwa kama mchezaji wa Super Eagles.