Savio yatoa kipigo cha mbwakoko kwa Segerea BC ligi RBA

Sunday June 16 2019

Mwanaspoti, Michezo, Mwanasport, Savio yatoa kipigo, cha mbwakoko, kwa Segerea BC ligi RBA

 

By Imani Makongoro

Dar es Salaam. Baada ya kusua sua katika mechi za awali za Ligi ya Mpira wa Kikapu mkoa wa Dar es Salaam (RBA), bingwa mtetezi Savio imemaliza mechi za mzunguko wa kwanza kwa kishindo.

Savio imehitimisha mchezo wake wa 15 na mwisho wa mzunguko wa kwanza kwa ushindi wa kishindo wa pointi 113-29 dhidi ya Segerea BC.

Bingwa huyo mara tatu mfululizo licha ya kufungwa michezo sita na kushinda tisa, amejinasua kutoka nafasi ya nane na kupanda hadi nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi hiyo kwenye mzunguko wa kwanza.

Wababe wengine wa Ligi hiyo, ABC imehitimisha mechi zake za mzunguko wa kwanza kwa kipigo cha pointi 59-40 dhidi ya Magnet.

Wakati Jogoo yenyewe ikihitimisha mzunguko wa kwanza kwa kipigo cha pointi 105-67 dhidi ya Vijana huku ikiweka rekodi ya kufungwa mechi zote 15 za mzunguko wa kwanza.

Jogoo ya mwisho katika msimamo ikiwa imefungwa michezo yote ikifuatiwa na Segerea BC na Youngstars ambazo ziko kwenye 'danger zone'.

Advertisement

Timu za Chui, Kurasini Heat, Tanzania Prison, Mabibo Bullets na Pazi zimejinasua kwenye 'danger zone' lakini haziko katika nafasi nzuri.

Wakati timu za JKT, Oilers, Vijana, ABC, Ukonga Kings, Savio, JKT Mgulani na Magnet zikimaliza mzunguko wa kwanza katika nane bora.

"Baada ya mechi za mzunguko wa pili, timu zitakazomaliza kwenye nane bora zitacheza play off (mtoano) ili kusaka bingwa mpya wa msimu huu," alisema Mkurugenzi wa ufundi wa Chama cha mpira wa kikapu Dar es Salaam (RBA), Gosbert Boniface.

 

Advertisement