Mbivu mbichi za sakata la Bocco kusaini Simba, Polokwane

Tuesday June 11 2019

 

By Imani Makongoro

Dar es Salaam. Mshambuliaji John Bocco amejiweka katika hatari ya kufungiwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) endapo atabainika alifanya udanganyifu kwa kutia saini katika klabu mbili tofauti Simba na Polokwane ya Afrika Kusini.

Habari za uhakika zilisema mshambuliaji huyo ametia saini mkataba wa awali na Polokwane usiku mara baada ya kumalizika mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambao ungeanza Julai Mosi 2019 hadi Juni 31, 2021.

Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori alidai Polokwane haikufuata utaratibu kwa kufuata Bocco kwanza badala ya klabu yake.

Kwa mujibu wa kanuni ya Fifa kuhusu usajili ya Bosman inasema mchezaji ambaye mkataba wake upo chinini ya miezi sita yupo huru kusajili mkataba wa awali na klabu nyingine unamruhusu kuondoka wakati dirisha la usajili litakapofunguliwa.

Akizungumzia sakati hilo la Bocco aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Saad Kawemba alisema Polokwane haikutakiwa kuzungumza na Simba usajili wa Bocco kwa kuwa wakati anatia saini mkataba wa awali ulikuwa ndani ya miezi sita ili amalize ule wa Simba.

"Alichotakiwa Bocco ni kuweka wazi kwa Simba kwamba mimi siongezi mkataba mwingine kwa kuwa tayari nina mkataba wa awali na Polokwane, lakini si Polokwane wazungumze na Simba kanuni haipo hivyo.

Advertisement

"Kama nyaraka zipo zinaonyesha Bocco alisaini mkataba wa awali na Polokwane, kisha akarudi kuongeza mkataba na Simba endapo Polokwane watalivalia njuga mchezaji anafungiwa," alisema Kawemba.

Kauli ya Magori

Akizungumzia utata huo Magori alisema Polokwane hawakufuata utaratibu walipompa mkataba wa awali Bocco.

"Tulijua Bocco amesaini mkataba wa awali lakini hilo halikutuzuia kumpa mkataba mpya kwasababu bado alikuwa katika mkataba na Simba.

"Polokwane walikosea kwa sababu hawakufata taratibu, walijua tayari tumeshamsaini lakini wao naona walikuwa wanataka kama ushindani na sisi, hata huyo wakala sisi tulimuambia kabisa kwamba tayari tumemalizana," alisema.

Alidai suala la mkataba wa awali hata wao walimsainisha mshambuliaji wa Ndanda, Vitalis Mayanga lakini sio mchezaji wao.

"Mkataba wa awali unakua unamuonyesha mchezaji uhakika wa yeye kuhitajika, hao Polokwane wamempa Bocco mkataba juu ya mkataba kitu ambacho wamekosea na kama Psl wamepokea mkataba basi Fifa itahusika," alisema.

Meneja wa Bocco, Jemedari Saidi alisema hajui mkataba baina ya mchezaji huyo na timu ya Polokwane anaoufahamu yeye ni ule wa Simba ambao walifanya mazungumzo Mei 13 mpaka Mei 17 ndipo wakasaini rasmi mkataba mpya.

"Labda aulizwe Bocco mwenyewe, lakini huo mkataba wa Polokwane siufahamu, kwa 'status' yangu nisingeweza kumsainisha mchezaji sehemu mbili, Bocco tangu amesaini Simba ni mwezi sasa unaelekea, huo wa Polokwane siufahamu, na alichokisaini siwezi kukisemea sababu sikijui" alisema.

Jana Simba walionyesha picha za mchezaji huyo akisaini huku akishuhudiwa na mwekezaji wa klabu hiyo, Mohamed Dewji (Mo) na meneja wa Bocco, Jemedali Said.

Katibu Mkuu wa zamani Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah aliungana na Kawemba akibainisha kwamba, mkataba wa awali unamfunga mchezaji ambaye mkataba wake katika klabu aliyopo unaelekea ukingoni.

"Mkataba ule unamaanisha kwamba, utakapoliza mkataba na klabu uliyopo ambao unakuwa ni ndani ya miezi sita lazima ujiunge na klabu uliyosaini mkataba wa awali.

"Bocco kama itagundulika alidanya kule Polokwane, atachukuliwa hatua za kinidhamu, lakini pia wakati akisaini Simba haki ya mdhamini haikuwepo, kwani haki ya mdhamini ni kila habari 'official' ya klabu, lakini wakati Bocco akisaini katika picha zilizotolewa na Simba, haikuwepo," alisema.

Manula, Kapombe wajifunga Simba

Katika hatua nyingine, kipa Aishi Manula na beki beki Shomari Kapombe wamesaini mikataba mipya kuendelea kuitumikia timu hiyo.

Habari za uhakika kutoka ndani ya klabu ya Simba zilibainisha kuongezwa miakata wachezaji hao, licha ya kuhofia kuweka wazi ni ya muda gani.

"Makubalino ya ndani ni kwamba habari zote zitatolewa 'official' hivyo kwa kifupi wachezaji hao wamekwishasaini Simba pamoja na Bocco (Mei 17), lakini mikataba ya muda gani, taarifa rasmi zitatolewa kulingana na makubaliano," alisema.

Magori alipoulizwa kuhusu kuongezwa mikataba wachezaji hao alisema zoezi la kuwaongezea mikataba wachezaji wao linaendelea kila siku tangu juzi.

"Hiki ni kipindi cha kuwaongeza mikataba wachezaji ambao tunabaki nao, kila kitu kitakuwa wazi na Leo saa 7 Mchana (Jana) tutamuongeza mchezaji mwingine mkataba, zoezi litafanyika kila siku hadi idadi tunayohitaji itakapotimia," alisema," Magori.

Alisema baada ya kuwaongeza mikataba, itatangaza wachezaji wanaoachwa, kisha wapya watakaosajiliwa kipindi hiki cha dirisha kubwa.

Advertisement