Bilo: Nataka kuondoka kwa amani Stand United

Monday June 10 2019

Mwanaspoti, Michezo, Bilo, Stand United, Yanga, Simba, Ligi Kuu, Soka

 

By OLIPA ASSA

Dar es Salaam. Baada ya Stand United 'Chama la Wana' kushuka daraja, kocha wao Athuman Bilali 'Bilo' amewaaga viongozi wa klabu hiyo.

Bilo amesema timu hiyo iliposhuka daraja aliwaambia viongozi kuwa yupo tayari kubaki kuhakikisha anaipandisha, lakini amedai baada ya kuona ukimya na ofa zimekuja mezani kwake ameona ni busara kuwafahamisha jambo hilo.

Bilo anasema leo Jumatatu anakutana na viongozi wa timu hiyo kuwaambia ofa aliyopata ili waweze kumpa mkono wa kwa heri kutokana na timu hiyo kukaa nayo kwa miaka mitano.

"Nitakuwa siyo mwingi wa shukrani kama nitaenda kusaini kimya kimya halafu uongozi wa Stand United uje uone kwenye vyombo vya habari.

"Nilikuwa tayari kubaki, lakini baada ya ukimya wao na mimi nimeletewa ofa nimeona siyo jambo baya kukaa nao mezani niwajuze kilichopo na tuagane kwa amani.

"Nimepata ofa mbili kutoka Ligi Kuu na moja ya Daraja la Kwanza, kati ya hizo ipo nitakayosaini, sijasaini kwasababu bado sijakaa na uongozi ambao sijui unawaza nini juu ya hilo," alisema Bilo.

Advertisement

Advertisement