Mbona iko hivi: Jipangeni Fainali ni kwa ajili ya kushinda, sio kucheza!

Sunday June 9 2019

Mwanaspoti, Fainali, ajili kushinda, sio kucheza, Taifa Stars, Samatta

 

By Ezekiel Kamwaga

KWA yakini sikumbuki ni nani hasa aliyeibuka na kauli hiyo ambayo imetengeneza kichwa cha habari cha makala haya, lakini ni kauli ambayo makocha wa michezo yote hupenda kuwaambia wachezaji wao.
Katika mechi ya fainali ya mashindano ya aina yoyote, jambo la muhimu zaidi ni kutwaa kombe kwa sababu ndiyo kitu pekee kitakachobakia katika historia.
Jose Mourinho hubandika ujumbe huu ukutani kabla ya mechi yoyote ya kutwaa kombe. Falsafa hii tayari imefanya kazi kwake; amecheza fainali mbili za Kombe la Mabingwa wa Ulaya akiwa na timu mbili tofauti –Inter Milan ya Italia na Porto ya Ureno na ametwaa ubingwa mara zote hizo.
Kauli hii maarufu ilinijia mara baada ya mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baina ya Liverpool na Tottenham zote za England.  Majogoo wa Anfield walishinda 2-0 na kutwaa ubingwa; safari hii ikiwa mara yao ya sita kufanya hivyo.
Hata hivyo, haukuwa ubingwa rahisi kwa Liverpool hususani kwa washabiki wao. Mechi ilikuwa ngumu na Spurs kwa kweli walitawala mechi ile kwa kiasi kikubwa.
Liverpool haikucheza vema kabisa. Hata hivyo, waliweza kucheza kwa akili na kushinda mechi pasipo kucheza vizuri. Hata hivyo, baada ya dakika 90, Liverpool ndiyo waliotawazwa kuwa mabingwa na historia itawakumbuka namna hiyo.
Hakuna ambaye atakumbuka namna Harry Winks, Mousa Sissoko na Christian Eriksen walivyotawala eneo la kiungo. Wala hakuna ambaye atakumbuka namna Tottenham walivyokuwa wakisambaza mpira wapendavyo kutoka kulia kwenda kushoto.
Kama ambavyo watu hawakumbuki tena samba la aina yake lililopigwa na Brazil mwaka 1982 wakati wa fainali za Kombe la Dunia. Ile Brazil hadi leo inatambulika kama kikosi bora kilichoshindwa kutwaa Kombe la Dunia.
Toninho Cerezo, mrefu kama Patrick Viera lakini mwenye udhibiti wa mpira na mapafu ya mbwa alionyesha dunia namna ya kuicheza nafasi ya kiungo wa ulinzi; wenyewe wanaita volante kwa mapozi na ushindani wa aina yake.
Pembeni yake akiwa na kiungo mchezeshaji Falcao ambaye siyo kwamba alikuwa mmoja wa viungo bora duniani wakati huo, lakini akiunganisha safu ya kiungo na ushambuliaji kwa madaha yasiyo kifani.
Kipenzi changu akawa Socrates. Huyu alikuwa ni mchezaji ambaye alihitimu shahada ya udaktari wa binadamu angali akiwa anacheza katika kiwango cha juu.
Wenyewe wakimwita daktari lakini uwanjani akiwa nyota mbele ya nyota wenzake. Kitambaa kichwani, ndevu za kufa mtu –mzuri kwa mipira ya juu na chini na akitumia miguu yote; Socrates alikuwa mchezaji wa kwanza duniani kujulikana kwa kutoa pasi pasipo kutazama.
Lakini ubingwa wakachukua Wataliano. Wala hawakuwa na supastaa wa kiwango cha hao niliowataja. Wao walikuwa na ngome ya chuma iliyoongozwa na Dino Zoff golini na walinzi wa maana kama Franco Baresi na Gaetano Scirea. Paolo Rossi aliyekuja kuwa mfungaji bora wa Italia alitolewa jela kwa ajili ya kwenda kusaidia taifa lake. Italia walikuwa na hali mbaya namna hiyo.
Lakini, historia inaikumbuka Italia kwa sababu ilitwaa Kombe. Hakuna historia inayojengwa na watu walioshindwa kwani mara zote huandikwa na washindi.
Cheza uchezavyo lakini mwisho wa siku, kwenye fainali kazi muhimu ni kushinda na si kucheza vizuri.
Taifa Stars yetu nayo inakwenda kucheza AFCON baadaye mwezi huu nchini Misri. Kwa Kiswahili, AFCON hii ya Misri tunaita Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika. Hizi ni fainali na maana yake haibadiliki hata kama ni Tanzania. Ni washindi pekee ndiyo ambao watakumbukwa.
Ile timu ya akina Leodger Tenga inakumbukwa tu kwa sababu ilikuwa ya kwanza na kuweka historia yake. Wengine watakaofuatia, wakiwamo wachezaji wa Stars wa safari hii na wengine watakaokuja, hawatakiwi kushiriki tu.
Wajiamini kwamba wanakwenda AFCON Misri kwa ajili ya kushinda mashindano au kufikia hatua ambayo itabidi kila mtu atupie jicho Tanzania kujua siri ya mafanikio yetu ni nini.
Ukweli ni kwamba, Watanzania hawatajali nani alipiga chenga ngapi.
Mwisho wa siku, watatamani matokeo mazuri ya kujisifia mbele ya Waafrika wenzao.
Historia inakumbuka washindi tu.

Advertisement