Barcelona, Valencia hapatoshi Kombe la Mfalme

Muktasari:

Mara ya mwisho Valencia kuwafunga Barcelona katika fainali za Copa delo Rey ilikuwa mwaka 1958 ambapo walishinda 3-0.

Dar es Salaam. Mabingwa watetezi wa Kombe la Mfalme, Barcelona wanashuka uwanjani kesho kukipiga  na Valencia katika fainali ya kombe hilo.

Kwa mashabiki wa soka nchini Tanzania mchezo huu utaoneshwa kupitia king’amuzi cha StarTimes katika chaneli ya ST World Football LIVE kuanzia saa 4:00 Usiku siku ya Jumamosi tarehe 25 Mei.

Chaneli ya ST World Football inapatikana katika kifurushi cha SMART kwa watumiaji wa Dish na kifurushi cha UHURU kwa wateja wa Antenna.

Rekodi inaonyesha Valencia hii ni fainali yao ya 16 katika Kombe la Mfalme huku wakiwa wamefanikiwa kulichukua mara 7 na kupoteza fainali 9.

Mara ya mwisho Valencia kuwafunga Barcelona katika fainali za Copa delo Rey ilikuwa mwaka 1958 ambapo walishinda 3-0.

Barcelona ambao wamenyakua kombe la La Liga kwa msimu huu bado wana kazi ya kuwaridhisha mashabiki wao ambao wana majonzi ya kutolewa kwenye ligi ya mabingwa baada ya kuongoza kwa goli 3 katika mchezo wa kwanza na kuruhusu goli 4 kwenye mchezo wa marudiano dhidi ya Liverpool.

Mbali na morali kuwa chini Barcelona wana orodha ndefu sana ya majeruhi ambao miongoni mwao ni wachezaji wa kikosi cha kwanza, mshambuliaji Luis Suarez, kipa Ter Stegen (maumivu ya goti), Ousmane Dembele (maumivu ya misuli ya nyuma ya goti ‘hamsring’) na kiungo wa kati Arthur (maumivu ya nyonga).

Barcelona bado wana kikosi kizuri licha ya majeruhi walionao. Nahodha Lionel Messi amekuwa kwenye kiwango bora kabisa msimu huu baada ya kupachika mabao 36 katika ligi na kuisaidia timu yake kushinda taji hilo.