Hizi hapa sheria mpya zitakazotumika katika soka msimu ujao

Muktasari:

Mabadiliko ya kisheria ya mchezo wa soka yatakayoanza msimu ujao huku mengine yakitarajia kuanzia kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya itakayopigwa Juni Mosi baina ya Liverpool na Tottenham Hotspur huko Madrid

London, England. Maisha yanakwenda kasi asikwambie mtu. Hata kwenye mchezo wa soka kwa sasa mambo yako mbio na msimu ujao kutakuwa na mabadiliko kibao ya kisheria yanayohusu mchezo huo.

Haya hapa mabadiliko ya kisheria ya mchezo wa soka yatakayoanza msimu ujao huku mengine yakitarajia kuanzia kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya itakayopigwa Juni Mosi baina ya Liverpool na Tottenham Hotspur huko Madrid.

1. Wachezaji wa timu pinzani hawataruhusiwa tena kukaa kwenye ukuta unaoanzia wachezaji watatu au zaidi wakati wa kupiga friikiki. Badala yake timu inayoshambulia kwa wakati huo wachezaji wake watahitajika kukaa walau umbali wa mita moja kutoka ulipo ukuta wa wapinzani wao.

2. Ule mpira wa goli kiki au friikiki ambao awali ilihitajika utoke nje ya boksi ndio uendelee, kwa sasa haitakuwa hivyo tena, mchezo utaendelea hata kama mpira ukiwa haujatoka nje ya boksi. Kitu ambacho kinapaswa mchezaji wa timu pinzani hatakiwi kuwa ndani ya boksi wakati mpira unapigwa.

3. Ule mpira wa kuanzishwa na mwamuzi sasa atarushiwa moja kwa moja golikipa kama mchezo utakuwa umesimama mpira ukiwa ndani ya boksi. Ikiwa nje ya boksi, mwamuzi atawapa mpira timu ya mwisho iliyokuwa imegusa mpira huo, lakini wachezaji wengine wa timu zote mbili watapaswa kuwa mbali kwa mita nne.

4. Kama timu inayoshambulia mchezaji wao mpira ukimgusa mkononi kisha akafunga au akatengeneza nafasi ya bao hata kama kwa bahati mbaya, bao litakalopatikana halitakubaliwa. Tukio la mpira kugusa mkono wakati mtu anaponyanyua mikono juu, itahesabika kuwa mpira umeshikwa, isipokuwa kama tu mpira huo umepigwa na mchezaji mwenzake. Mpira wa kushika utahesabika kama tu mchezaji atajitanua kuliko ukubwa wa umbo lake kisha akarusha mikono na kuguswa na mpira.

5. Kwenye penalti, kipa kwa sasa ataruhusiwa kuweka mguu mmoja tu kwenye mstari wa goli wakati penalti inapigwa, mguu mwingine ataamua mwenyewe pa kuuweka. Lakini, makipa kwa sasa hawataruhusiwa kugusa mwamba au nguzo ya goli kabla ya penalti hiyo haijapigwa.

6. Mchezaji anayefanyiwa sub kutoka uwanjani atapaswa kutokea popote pale palipo karibu na si tena kwenda kutokea katikati ya uwanja kama ilivyo kwa sasa. Hii itapunguza suala la wachezaji kupoteza muda wanapofanyiwa mabadiliko.

7. Makocha na mameneja sasa watakuwa wanaonyeshwa kadi za njano na nyekundu wanapofanya makosa ya kinidhamu.

8. Timu iliyoshinda pale kwenye tukio la kurusha shilingi kabla ya mechi kuanza, yenyewe ndiyo itakayoamua kama ianze mpira kipindi cha kwanza au kwenye kipindi cha pili.

9. Mabadiliko kwenye kanuni za Uefa, wachezaji hadi 12 wa timu moja wataruhusiwa kukaa kwenye benchi na hiyo itaanzia kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu. Ligi Kuu England itaendelea kubaki na utaratibu wake wa kuwa na wachezaji saba kwenye benchi.

HIKI KITU SIO KWELI

Kuna baadhi ya magazeti ya Ulaya yamekuwa yakiripoti rebaundi hairuhusiwi tena kwenye penalti.

Jambo hilo lilijadiliwa na wahusika wa kupanga kanuni na sheria za mchezo wa soka, lakini lilikataliwa katika hatua za awali kabisa hata kwenye kupigiwa kura halijafika. Kama kipa atapangua penalti hiyo au ikagonga mwamba, wakati wa mchezo wa kawaida, hapo mchezo unaokuwa unaendelea, hivyo ribaundi inaruhusiwa.