Kajala: Acheni hizo buana

Muktasari:

Kajala ni miongoni mwa mastaa wa Bongo Movie waliokuwa kwenye tamthiliya ya Kapuni ambayo ilibamba kinoma.

Dar es Salaam.Ukimya wa supastaa wa Bongo Movie, Kajala Masanja, umewashtua mashabiki wake na kuanza kumsaka huko kwenye mitandao ili kufahamu kulikoni hashushi ngoma mpya.

Inaelezwa kwa muda mrefu sasa filamu mpya za Kajala hazionekani, hivyo baadhi kudai kwamba, ameanza kuitupa mkono tasnia kutokana na kubamba dili kibao za matangazo.

Hata hivyo, mwenyewe amewasikia na kuwapasha kuwa kamwe hawezi kuacha fani yake hiyo hata kama anabamba dili tamu.

Kajala, ambaye amekuwa gumzo huko kwenye mitandao kutokana na kurusha mapicha picha ya utata akiwa na mwanaye Paula, alisema kuwa haacha kuigiza na kuwa bado anaendeleza libeneke.

Alisema mashabiki wake wasiwe na mashaka kwani, kwa sasa mbali na filamu pia, amejikiza kwenye tamthiliya.

Kajala ni miongoni mwa mastaa wa Bongo Movie waliokuwa kwenye tamthiliya ya Kapuni ambayo ilibamba kinoma.

“Hata kama soko la sanaa ni gumu kwa sasa, lakini bado siwezi kuacha kuigiza na sasa nafanya sana tamthiliya kama ilivyo ya Kapuni ambayo imeisha hivi karibuni,” alisema Kajala.