Man City ya Guardiola NI ubingwa wa Ulaya tu

MANCHESTER, ENGLAND

PEP Guardiola amesema kamwe Manchester City haitahesabika kuwa ni bora duniani kama itashindwa kufanikiwa kubeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kuna mjadala umeibuka tangu walipobeba Ligi Kuu England kwa msimu wa pili mfululizo, wakikusanya pointi 198 kwenye misimu hiyo miwili, kitamkwe kwamba kikosi hicho cha Guardiola ni moja ya timu bora kabisa duniani.

Kam Man City watakuwa wamewafunga Watford uwanjani Wembley jana Jumamosi watakuwa wamebeba taji la Kombe la FA na hivyo kuwa timu iliyobeba mataji yote matatu ya ndani huko England baada ya kutanguliwa kubeba lile la Kombe la Ligi na la Ligi Kuu England.

Lakini, Kocha Guardiola amedai kwamba bado wana kazi kubeba taji kubwa zaidi, Ligi ya Mabingwa Ulaya ili kuhesabika kuwa timu moja na kuwa na thamani kama wanayopewa Manchester United waliposhinda mataji matatu ndani ya msimu mmoja mwaka 1999.

Au kama timu ya Liverpool iliyotawala Ulaya mwishoni mwa miaka ya sabini na mwanzoni mwa miaka ya themanini.

“Huwezi kushinda na historia, wao historia yao ni kubwa sana. Sidhani kama sisi ni bora zaidi, tunahitaji kupambana zaidi,” alisema Guardiola.

“Ni jambo zuri kama watu watatuweka kwenye chungu kimoja na timu hizo, lakini pengine itakuwa sahihi kama tukishinda Ligi ya Mabingwa Ulaya.

“Kwenye historia ya Ligi Kuu England, kwa upande wa matokeo, mabao na pointi, sisi ni bora. Lakini, soka sio mchezo wa namba tu. Sio mchezo wa takwimu tu, ni mchezo wa hisia na kuwagusa watu.

“Siwezi kusema sisi ni bora wakati kuna mtu kama Sir Alex Ferguson alivyoweza kutengeneza hisia za mashabiki wa Man United au Liverpool na Bob Paisley huko kwenye miaka ya themanini.

“Tutajaribu, lakini sidhani kama ni sahihi kujiita sisi bora kwa sasa. Sijui itachukua muda gani kuwa na kundi hili la wachezaji, lakini ndiyo hivyo kwenye soka watu lazima wajadiliane.

“Kuwekwa kwenye kundi moja na timu hizo zinazotajwa kuwa bora kabisa ni jambo zuri. Hatukuwa kwenye mawazo hayo wakati nilipowasili hapa. Lakini, kwa sasa watu wanafurahia kututazama tukicheza, nyumbani na ugenini.”

Wakati mashabiki wa timu hiyo wakionekana kutokujali kuhusu Ligi ya Mabingwa Ulaya na watafurahi tu kwa kubeba mataji matatu ndani ya msimu mmoja, Guardiola mpango wake ni kushinda taji hilo la Ulaya ili kuiweka klabu kwenye chati za juu kabisa.

Katika misimu mitatu ya Guardiola kwenye timu hiyo, Man City imeishia hatua ya 16 bora mara moja na robo fainali mata mbili, huku msimu huu wakishindwa kuingia nusu fainali baada ya kutupwa nje na Tottenham Hotspur. Kutokana na hilo, kocha huyo wa zamani wa Barcelona na Bayern Munich hajihesabii kama atakuwa amefanya kazi bora kabisa kwenye kikosi cha Man City kama atashindwa kuwapa raha ya kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Guardiola alisema: “Tunataka kulifanya hilo. Hiyo ndiyo ndoto yetu. Lakini, ni lazima nibadilike na kuwa bora zaidi, lazima nijitathmini juu ya nini nifanye kufanikiwa hilo. Sijawahi kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya nikiwa na Man City.

“Ni michuano migumu. Ni michuano isiyotabirika na imekuwa ikichezwa kwa hisia sana kuliko michuano mingine. Unakuwa na mawazo, naenda kutolewa au naenda kushinda. Ukifanya kosa tu, unaadhibiwa hapohapo. Kwenye ligi za ndani jambo hilo sio mara nyingi kutokea.”

Guardiola alizungumzia pia kuhusu msimu ujao na kudai anaamini Liverpool watarudi wakiwa na hasira na hawatakuwa wavumilivu wa kuendelea kusubiri kwa miaka 30 bila ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England.

Guardiola aliisaidia Man City kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu England na kuwa kocha wa kwanza kufanya hivyo katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

“Nadhani hata Chelsea, Manchester United, Arsenal na Tottenham nao watarudi kwa nguvu mpya msimu ujao,” alisema.