Mogella aipa Simba ujanja wa kuimaliza TP Mazembe kwao

Muktasari:

Mashabiki wa Simba ni kama wamekata tamaa ya kutinga hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutoka suluhu na TP Mazembe.

Dar es Salaam. Simba wanakipiga na TP Mazembe kesho Jumamosi ni mechi ngumu zaidi kwao baada ya kushindwa kutumia vyema uwanja wao wa nyumbani, pamoja na hayo nyota wa zamani wa timu hiyo, Zamoyoni Mogella amewapa mbinu za kupindua matokeo.

Mogella anaamini bado Simba ina nafasi ya kwenda kuwaduwaza TP Mazembe, akisema hilo lipo mikononi mwa mastaa wa kikosi hicho, kucheza kwa nidhamu na kujitoa basi watakuwa wamemaliza kazi.

"Unapozungumzia nidhamu sio ile ya kuwaogopa TP Mazembe, bali ni kuzitumia kikamilifu nafasi ambazo watazipata, wajitume, kila mtu asimamie majukumu yake asilimia 100.”

"Kinachowasumbua wachezaji wengi, wanapungukiwa na uzalendo wa kujituma, wajifunze kwa timu za nje wanapopoteza wanakuwa watu wa kuonyesha uhitaji wa kushinda na ndio maana hata TP Mazembe wenyewe wana mafanikio.

"Pia, akili zao zitambue kwamba wanaenda kucheza na binadamu kama wao na sio malaika kwamba wanajifunza mpira juu ya aridhi," alisema Mogella.